Lubanga ahukumiwa kifungo cha miaka 14
10 Julai 2012Hakimu Adrian Fulford aliitangaza hukumu ya Lubanga na kueleza kwamba mshtakiwa huyo atakwenda jela kwa miaka 8 tu kwa sababu ameshakaa rumande tangu mwaka 2006. Lubanga mwenye umri wa miaka 51 amehukumiwa kwa kosa la kuwateka watoto wadogo, baadhi yao wakiwa na umri wa miaka 11 tu, na kuwatumia kama maaskari katika kundi lake la waasi. Hata hivyo hakimu Fulford amesema kwamba mahakama imeshindwa kuthibitisha kwamba Lubanga alihusika katika shutuma za unyanyasaji wa kijinsia.
Lubanga alikuwa mtu wa kwanza kufikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya ICC, akishtakiwa kwa makosa kadha wa kadha yanayokiuka haki za binadamu. Tarehe 14 mwezi Machi mwaka huu, mahakama ilitangaza kwamba Lubanga amekutwa na hatia ya kuwakamata watoto na kuwatumia kama maaskari katika mapambano yaliyofanyika kwenye eneo la Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo kati ya mwaka 2002 na 2003.
Mwendesha mashtaka aliomba kifungo cha miaka 30
Katika kuamua adhabu ya kumpa Lubanga, mahakama ilizingatia uzito wa makosa aliyoyafanya, hali yake binafsi pamoja na kuangalia mazingira ambamo uhalifu huo ulifanyika ili kutathmini kama anastahili kupewa adhabu ya juu zaidi au ndogo. Kulingana na sheria za ICC, kiwango cha juu cha kifungo anachoweza kupewa mshtakiwa ni miaka 30. Mahakama hiyo inaweza pia kumtoza mshtakiwa faini. Katika kesi ya Lubanga, mwendesha mashtaka mkuu wa zamani, Luis Moreno-Ocampo, aliomba apewe kifungo cha miaka 30.
Akizungumza na Deutsche Welle, Bi Géraldine Mattioli-Zeltner, ambaye ni kiongozi wa kitengo cha kupigania haki ya kimataifa kutoka shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, alisema: "Ipo mifano ya kesi katika mahakama maalum ya Sierra Leone ambapo baadhi ya waasi waliohukumiwa kwa kosa hilo walipewa kifungo cha miaka kati ya 35 na 52. Lakini kiwango cha juu cha adhabu katika mahakama hiyo ni kikubwa zaidi kuliko ICC."
Lubanga anaweza kukata rufaa iwapo atakuwa hajaridhika na uamuzi wa mahakama. Bosco Ntaganda, ambaye ameshtakiwa pamoja na Lubanga, bado anaendelea kuukwepa mkono wa sheria. Hata yeye anatafutwa na mahakama ya ICC kwa kosa la kukamata watoto na kuwafanya kuwa maaskari katika mapambano ya Ituri kati ya mwaka 2002 na 2003.
Hukumu ya Lubanga yachukuliwa kama ishara muhimu
Hivi karibuni, mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo alitoa warranti wa pili wa kukamatwa kwake kwa kosa la kushiriki katika vitendo vya mauaji, utekaji nyara, uporaji na ubakaji yaliyofanywa na kundi la waasi wa Union of Congolese Patriots. Mwaka 2009, Ntaganda alipewa kibali cha kujiunga na jeshi la Congo na kupewa cheo cha jenerali. Hata hivyo, mwezi machi mwaka huu alilikimbia jeshi na kuanzisha vurugu katika eneo Kivu ya Kaskazini, lililo Mashariki mwa Congo.
Akiuzungumzia umuhimu wa hukumu dhidi ya Lubanga, Géraldine Mattioli-Zeltner wa shirika la Human Rights Watch amesema: "Ninaamini kwamba ina umuhimu mkubwa, hasa kwa wahanga wa uhalifu uliofanywa na Lubanga, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri haki itendeke. Mwezi Machi alikutwa na hatia lakini hukumu ya leo itakuwa ishara yenye nguvu kwa watoto hawa kwamba haki imetendeka. " Aliongezea kuwa shirika lake linaamini kwamba itakuwa ishara kwa wengine wote wanaoendelea kukamata watoto na kuwafanya maaskari na itaonyesha uzito wa uhalifu huo na kuwa onyo kwa wote wanaoendelea na shughuli hiyo.
Kesi ya Lubanga ilianza kusikilizwa mwaka 2009 na imeshaendeshwa kwa jumla ya siku 204. Katika kipindi hicho zaidi ya mashahidi 60 walifika mahakamani kutoa ushahidi wao.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp
Mhariri: Mohammed Khelef