1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lufthansa yafuta karibu safari zote za ndege sababu ya mgomo

Sylvia Mwehozi
27 Julai 2022

Shirika la ndege la Ujerumani la Lufthansa limetangaza kufuta zaidi ya safari za ndege 1,000 katika viwanja vya Frankfurt na Munich katika siku zijazo kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa ardhini uliotangazwa kuanza leo.

Lufthansa
Picha: Daniel Kubirski/picture alliance

Kwenye taarifa yake, Lufthansa imesema mgomo huo wa siku moja ulioitishwa na chama kikubwa cha wafanyakazi cha Verdi, utakuwa na "athari kubwa".

"Lufthansa itapaswa kufuta karibu programu nzima ya safari za ndege katika viwanja vikuwa vya Frankfurt na Munich siku ya Jumatano", imesema taarifa hiyo ikiongeza kuwa safari zilizopagwa Alhamis na Ijumaa huenda nazo zikaathiriwa.

Zaidi ya safari za ndege 1,000 zitafutwa ikiwemo baadhi ambazo zimeondolewa tangu jana na kuathiri abiria karibu 134,000.

Chama kikubwa cha wafanyakazi wa Ujerumani Verdi, ambacho kinawakilisha wafanyakazi wa ardhini 20,000 wa Lufthansa kinataka nyongeza ya asilimia 9.5 ya mshahara. Kimesema mapendekezo ya sasa ya utawala hayakidhi mfumuko wa bei ambao ulifikia asalimia 7.6 nchini Ujerumani mwezi uliopita. 

Lufthansa imepinga madai hayo ikisema kwamba imetoa "ongezeko kubwa la mishahara" linalofikia zaidi ya asilimia 10 kwa wafanyakazi katika makundi ya mishahara ya chini na ongezeko la asilimia sita kwa wafanyakazi wanaolipwa zaidi.

Mgomo huo unafanyika wakati familia nyingi zikiwa katika likizo za majira ya joto. 
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW