Lugha na jinsia
29 Desemba 2009Lugha mara nyingi huashiria maadili na mienendo ya jamii yoyote ile. Wasomi katika falsafa ya sayansi ya jamii kwa muda mrefu wamesisitiza kwamba lugha ndio kioo na chanzo cha kutambulisha utamaduni wa jamii. Lakini, je ni mabadiliko yapi yanayojitokeza katika matumizi ya lugha hasa kwa kuashiria vyeo vya wanawake wanaoshikilia nyadhifa za uongozi wa juu?
Ili kuwa na urari na muwala, Lugha nyingi hubadilisha jinsia ili kutopoteza maana katika matamshi na sentensi. Katika kiItaliano, kwa mfano, wanawake wengi hupenda kutumia majina ya vyeo vya kiume kwa sababu vile vyeo vya kike mara nyingi huchukuliwa kwa kejeli na makaripio.
Dhana hii ya matumizi ya lugha huzua vipengee vya ubishi wa ufasaha wa lugha na usahihi, kijamii.
Angelika Mucchi-Faina, ambaye ni Profesa wa Saikolojia katika chuo kikuu cha Perugia, nchini Italy, anadai kuwa tatizo si la lugha bali ni kule kutohamasishwa jamii kuhusu majukumu ya wanawake katika jamii inayoendelea kupevuka. Anakiri kuwa kwa miongo kadhaa iliyopita hatamu ya uongozi katika sekta ya umma imekuwa ikitengewa wanaume, kasumba ambayo anadai bado inaathiri fikra na matamshi ya watu na kuendelea kuwadhalilisha wanawake.
Kimsingi, lugha ya kiingereza, kwa mfano, haitumii jinsia katika matumizi yake, ilhali lugha zinginezo, kama Kiitaliano, Kihispania na pia Kijerumani, zinatofautisha majina kwa jinsia, ikiwemo kike na kiume.
Profesa Jose Luis Jimenez, mwana isimu katika chuo kikuu cha Zaragoza, Italia, anadai kuwa ubaguzi huu wa lugha dhidi ya wanawake unakithiri zaidi kutokana na mitindo ya matamshi ya lugha mbalimbali na ishara zenye maana fiche kijamii.
Kwa mfano, katika matumizi ya lugha na vyeo, Kiitaliano, 'il ministro mara carfagna' ni tafsiri ya --waziri wa usawa wa kijinsia-- …na mara nyingi inakosa maana ikiwa ni mwanamke ndiye waziri husika. Mfano huu ni sawia na matumizi ya 'mwenyekiti' …tafsiri ya 'chairman' katika Kiingereza na hutumika pia kuwataja wanawake wenyekiti.
Nchi kadhaa, ikiwemo Italy mwaka wa 1986, zimejaribu kuondoa matumizi ya jinsia katika matamshi ya lugha, jambo ambalo baadaye hukaripiwa na hatimaye kusahaulika, hivyo kuipa lugha na wazungumzaji uhuru wa kujieleza pasipo kujali kero na utata unaozuka kuhusu haki ya kijinsia.
Lakini mwanasiasa Luisa Capelli wa chama cha 'Italia die valori' yaani chama cha maadili, anapendekeza kuwa ni heri matumizi ya tangu jadi ya jinsia ya kiume kuendelezwa ili jinsia ya kike ipate kutumiwa bila kufanyiwa kejeli.
Haya ni katika mantiki kwamba Wana-isimu wanadai kinachozungumziwa sana hadharani na faraghani, mwishowe huenda kikabadilishwa na kusalia bure, bila ya hatua yoyote ya mabadiliko kuchukuliwa.
Jinsia na athari yake katika matumizi ya lugha ilichipuka kama tatizo, wakati wa kongamano la dunia kujadili hadhi ya wanawake nchini Mexico mwaka wa 1975. Baada ya mapendekezo kuratibishwa mwaka wa 1989, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni , UNESCO; lilichapisha kijitabu cha vielelezo vya uandishi kinachozuia matumizi ya jinsia ya lugha baguzi kama njia ya kutoa mwongozo kwa waandishi wa fasihi simulizi na andishi.
Nchi nyingi wanachama, ikiwemo Italia na Uhispania, hazikuchukulia mapendekezo hayo kwa uzito unaofaa. Kitabu kingine cha maagizo ya matumizi ya jinsia isiyobagua; maarufu kama 'Non-sexist administrative manual' ‚ kilichochapishwa mwaka wa 2002 na kitengo cha maswala ya wanawake katika chuo kikuu cha Malaga, Uhispania, kilitafiti kuwa 'lugha hukua kulingana na matarajio na mahitaji ya jamii na kwamba katika jamii kama ya sasa inayopigia debe usawa wa kijinsia, lugha bila shaka itatumiwa kama chombo cha mabadiliko na pia kielelezo cha usawa.
Profesa Aliaga Jimenez hata hivyo anasisitiza kuwa wale wasiojua historia ya lugha ndio huenda wakakerwa zaidi na matumizi tata ya jinsia na matamshi.
Na pia kulingana na Irene Giacobbe kutoka katika taasisi ya nguvu ya jinsia, Italia ni nchi isiyokuwa na wanawake wengi wanaoshikilia nyadhifa za uongozi wa ngazi ya juu na hivyo anakiri kuwa usawa wa kijinsia utapatikana ikiwa jamii itazingatia usawa wa kijinsia wa matamshi ya lugha, la sivyo mjadala huu utasalia gumzo tu ...bila mbinu mbadala wa kuboresha uhusiano baina ya wake na waume…kijamii na kilugha.
Mwandishi: Peter Moss/IPS
Mhariri: Miraji Othman