1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Luis Enrique atangaza kikosi cha Uhispania

Sekione Kitojo
31 Agosti 2018

Luis Enrique kocha  mpya  wa  timu  ya  taifa  ya  Uhispania ametangaza  kikosi  chake kwa  kushangaza baada  ya kuwaacha kando  wachezaji  wa  kawaida  kama Jorge "Koke" Resurreccion, Jordi Alba  na  lago Aspas.

Spanien Fußball Trainer Luis Enrique
Picha: Getty Images/Bongarts/M. Hangst

Enrique amewaita  wachezaji  24 kwa  ajili  ya  michezo  ya  timu hiyo  dhidi  ya  England  na  Croatia  katika  ligi  ya  mataifa.

Kocha  huyo  wa  zamani  wa  Barcelona  amewajumuisha  wachezaji 13 kutoka  kikosi kilichocheza  katika  kombe  la  dunia, ikiwa  ni pamoja  na  David de Gea, Sergio Ramos, Sergio Busquets  na Diego Costa.

Mlinzi wa Uhispania Sergio RamosPicha: Getty Images/AFP/M. Riopa

Miongoni  mwa  wale  wanaorejea  katika  kikosi  hicho baada  ya kukosa  nafasi  katika  kikosi  kilichokwenda  katika  kombe  la  dunia ni  pamoja  na  Alvaro Morata na  Sergio Roberto.

Andres Iniesta , Gerard Pique  na  David Silva  tayari  walitangaza kujiuzulu  kutoka  timu  hiyo ya  taifa  kufuatia  kuondolewa  kwa Uhispania  na  wenyeji  wa  mashindano  hayo  Urusi  katika  duru ya  timu  16.

Kocha  wa  mpito Fernando Hierro alikuwa  akikifundisha  kikosi  cha Uhispania  katika  kombe  la  dunia kwasababu Julen Lopetegui alifukuzwa  siku  mbili  kabla  ya  kuanza  kwa  mashindano  hayo  ya kombe  la  dunia  kwa  kukubali  kazi  ya  kuifunza  Real Madrid bila ya  kuwaambia  maafisa  wa  shirikisho  la  kandanda  la  Uhispania.

Mmoja kati ya wachezaji waliotangaza kujiuzulu katika kikosi cha Uhispania David Silva (kulia)Picha: Reuters

Enrique  hakuzungumzia  juu  ya  wachezaji  aliowaacha  na  kusema "mshangao  zaidi" unatarajiwa  hapo  baadaye.

Kocha  huyo  amemjumuisha katika kikosi  chake   mlinzi  Diego Lllorente  licha  ya  kuwa  hataweza  kucheza  kutokana  na kufanyiwa  upasuaji  katika  mguu  wake  wa  kushoto uliovunjika.

Enrique  amesema  mlinzi  huyo  mwenye  umri  wa  miaka  25 anaonekana  kuwa  mchezaji  mzuri  sana  hapo  baadaye na anataka  kupata  uzoefu wa  kuwa  pamoja  na  wachezaji  wengine katika  timu  ya  taifa. Uhispania  inacheza  na  England Septemba  8 na  wenyeji  Croatia  siku  tatu  baadaye.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW