Lukashenko aonya kuchukua hatua kali dhidi ya waandamanaji
10 Agosti 2020Lukashenko aliwaeleza waandamanaji kuwa ni kama kondoo wanaotumiwa na mabwana zao kutoka nje.
Watu kadhaa wamejeruhiwa na maelfu wamekamatwa saa kadhaa baada ya uchaguzi uliofanyika jana Jumapili, wakati polisi walipovunja kikatili maandamano ambayo wengi walioshiriki walikuwa ni vijana kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi na maguruneti ya kushitua. Wanaharakati wa makundi ya haki za binadamu wamesema mtu mmoja alifariki baada ya kukanyagwa na gari ya polisi, kitu ambacho maafisa hao wamekana.
Maafisa wa uchaguzi wamesema jana kuwa Lukashenko ameshinda muhula wa sita madarakani kwa asilimia 80 ya kura, wakati mgombea wa upinzani Sviatlana Tsikhanouskaya amepata asilimia 9.9. Tsikhanouskaya ameyakataa matokeo hayo rasmi kuwa ni udanganyifu na kuapa kupambana kupinga matokeo hayo, na upinzani unapanga maandamano mapya katika mji mkuu Minsk, pamoja na miji mingine baadaye leo. Tsikhanouskaya amesema.
"Kile kilichotokea jana ni makosa ya serikali. Tumewaomba wasitumie nguvu dhidi ya watu ambao wameingia mitaani. Inauma. Na leo tumewafahamisha kwamba mtu mmoja amefariki, lakini kwa sababu hatuna intaneti, hatuwezi kuthibitisha ama kukataa. Nina matumaini sio kweli na wote wako salama."
Ukandamizaji wa kikatili
Ukandamizaji huo wa kikatili wa polisi umesababisha ukosoaji mkubwa kutoka mataifa ya Ulaya na bila shaka utasababisha hali tata ya juhudi za Lukashenko kuweka mahusiano mazuri na mataifa ya magharibi mnamo wakati kuna hali ya wasiwasi na mshirika wake wa karibu na mfadhili, Urusi.
Lakini Lukashenko , ambaye utawala wake wa mkono wa chuma wa miaka 26 umesababisha hali ya kutokuridhika katika taifa hilo la iliyokuwa umoja wa kisovieti lenye wakaazi milioni 9.5, ameonya kuwa hatasita kutumia nguvu tena kuyatawanya maandamano ya wapinzani. Amedai kuwa waandamanaji walikumbana na jibu sahihi usiku baada ya kuwajeruhi maafisa 25 wa polisi na kujaribu kuchukua udhibiti wa majengo ya serikali katika miji kadhaa ya Belarus.
"Hatutawaruhusu kuivuruga nchi yetu ," amesema. "tulitaka kuifanya siku hii kuwa ni ya mapumziko kwa watu. lakini baadhi walitaka kuharibu siku ya mapumziko."
Mkurugenzi huyo wa zamani wa mashamba ya serikali mwenye umri wa miaka 65 amedokeza kwamba upinzani unaongozwa kutokea Poland na Jamhuri ya Cheki, na kuongeza kuwa baadhi ya makundi nchini Ukraine na Urusi huenda pia yalikuwa nyuma ya maandamano hayo.