Lula da Silva afikishwa gerezani baada ya kujisalimisha
8 Aprili 2018Matangazo ya moja kwa moja ya vituo vya televisheni vya Brazil yameonesha akiwasili kwa helikopta katika makao makuu ya polisi katika mji wa Curibita ulioko kusini mwa Brazil. Hayo yanakuja baada ya Lula da Silva kujisalimisha kwa polisi.
Katika hotuba iliyojaa hisia aliyoitoa mjini Sao Bernardo do Campo kabla ya kujisalimisha, Lula amejitaja kuwa raia aliyeghadhbishwa kuhusiana na mashitaka hayo ya ufisadi akimshutumu jaji Sergio Moro kuwa alidanganya kumuhusu kuwa alipewa jengo na kampuni moja ya ujenzi kama rushwa.
Je ni kuporomoka kwa enzi ya Lula?
Helikopta iliyokuwa imembeba ilipotua, waandamanaji waliokuwa wamekusanyika nje walifyatua fataki, huku polisi nao wakitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya. Watu wanne wamejeruhiwa katika vurumai hilo.
Kabla ya kuwasili Curitiba, mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 72 aliondoka Sao Paolo akiwa amezingirwa na walinzi kwenye jengo la muungano wa wafuaji vyuma mjini humo, alipenya katikati ya wafuasi wake waliokuwa wanamzuia asiondoke na kuingia katika gari la polisi. Anasisitiza kuwa mashitaka dhidi yake yalichochewa kisiasa.
Lula alikutwa na hatia ya kupokea rushwa kutoka kwenye kampuni kubwa ya ujenzi, ili iweze kupata mikataba ya serikali. Makosa ya kuhusika na rushwa ni jambo lenye uwezekano mkubwa wa kuhitmisha maisha yake kisiasa na matumaini ya kurudi tena madarakani.
Licha ya kashfa zinazomkabili, Lula anaongoza kwa umaarufu kulingana na utafiti wa maoni ya wapiga kura kuelekea uchaguzi wa rais nchini Brazil unoatarajiwa mwezi Oktoba mwaka huu. Amejaribu kuchelewesha hukumu dhidi yake kwa kukataa rufaa mara kadhaa katika mahakama ya juu bila ya mafanikio.
Siku ya Ijumaa, jaji wa mahakama kuu alikuwa amemtaka Lula kujisalimisha kwa polisi ifikapo saa kumi na moja jioni lakini alikiuka muda huo uliowekwa wa kujisalimisha. Jumamosi, maelfu ya wafuasi wake walimsihi asijisalimishe na kumzuia kuondoka kutoka majengo ya chama cha wafanyakazi wafua vyuma.
Lula ni mwanasiasa maarufu Brazil
Baada ya kukamatwa na polisi, maandamano kutoka kwa wafuasi wake na sherehe kutoka kwa wanaompinga zilishuhudiwa katika miji ya Brasilia, Rio de Janeiro, Sao Paulo na miji mingine. Wapinzani wake wanamuona kuwa ndiye anawajibika kwa misururu ya kashfa za ufisadi zinazoikabili siasa za Brazil.
Lakini wafuasi wake wamesononeka kwa kuondoka katika ulingo wa siasa wa kiongozi wanayemkumbuka kwa kuwaondoa mamilioni ya watu kutoka kwa umasikini.
Wakati wa utawala wake, Lula ambaye anaenziwa sana katika historia ya Brazil na katika siasa za mrengo wa kushoto duniani alifanikiwa kuliunganisha taifa na kuimarisha uchumi wa taifa lake.
Baada ya kuhukumiwa na kuanza kutumikia kifungo cha miaka 12 jela, kinyang'anyiro cha urais mwezi Oktoba sasa hakiwezi kutabirika ni kiongozi yupi ataibuka kuwa na uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa wapiga kura kama Lula.
Lula ameishutumu idara ya mahakama na vyombo vya habari nchini humo kwa kumuandama ili kumzuia kugombea urais.
Hata hivyo huenda akapata afueni ya kisheria ifikapo Jumatano wiki ijayo baada ya vyombo vya habari Brazil kuripoti kuwa mahakama ya juu huenda ikatathmini upya sheria ya sasa kuhusu kufungwa kwa mshukiwa wakati amewasilisha kesi ya kukataa rufaa.
Kuna shinikizo la kubadilisha sheria ili kuwaruhusu washukiwa kuwa huru wakati kesi zao za kukata rufaa bado zinashughulikiwa na mahakama hiyo ikimaanisha iwapo mabadiliko hayo ya kisheria yataidhinishwa basii Lula atakuwa huru kusubiri hatma ya rufaa.
Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters
Mhariri: Jacob Safari