LUSAKA : Chiluba azuiliwa kwenda Zimbabwe
16 Aprili 2005Serikali ya Zambia imemzuwiya Rais wa zamani wa nchi hiyo Fredrick Chiluba ambaye anakabiliwa na mashtaka ya rushwa kuhudhuria sherehe za siku ya taifa katika nchi jirani ya Zimbabwe.
Chiluba ni miongoni mwa wakuu wa zamani kadhaa wa nchi wa Afrika walioalikwa na Zimbabwe kuhudhuria sherehe za miaka 25 ya uhuru wa nchi hiyo.
Emmanuel Mwamba msemaji wa Chiluba amesema serikali imegoma kumpa paspoti yake Rais huyo wa zamani ili kumuwezesha kuondoka nchini humo kwa ajili ya kuhudhuria sherehe hizo za uhuru nchini Zimbabwe.
Pasi ya kusafiria ya Chiluba ilitaifishwa baada ya kukamatwa kwa madai ya rushwa,wizi wa fedha za umma na kutumia vibaya madaraka yake baada ya kuiongoza nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 2001.
Mwamba amesema awali serikali ilikataa kugharamia safari hiyo nchini Zimbabwe lakini wakati Chiluba alipodokeza kwamba atajigharimia mwenyewe binafsi wamegoma kumpatia paspoti yake hiyo.
Hii ni mara ya tatu kwamba Chiluba amezuiliwa kusafiri na serikali.