LUSAKA : China kuwekeza dola milioni 800 Zambia
4 Februari 2007Serikali ya Zambia imesema hapo jana China itawekeza upya nchini humo dola milioni 800 na imekipiga marufuku chama kikuu cha upinzani kushiriki katika matukio ya kuadhimisha ziara ya Rais Hu Jintao wa China nchini humo kutokana na msimamo wa chama hicho dhidi ya China.
Zambia imeshuhudia machafuko kutokana na kuongezeka kwa nguvu za China barani Afrika ikiwa ni pamoja na ghasia kuhusiana na malipo katika mgodi mmoja unaomilikiwa na China.Chama cha upinzani cha Patriotic Front kimekuwa kikishutumu serikali kwa kuiuza nchi hiyo kwa China.
Rais Levy Mwanawasa wa Zambia baada ya kukutana na Rais Hu Jintao amesema China itawekeza dola milioni 800 kwa uchumi wa Zambia na kwamba serikali itaanzisha kanda maalum ya uchumi kwa ajili ya makampuni ya China.
Uwekezaji wa fedha hizo za China utakuwa katika migodi, uzalishaji wa bidhaa viwandani na kwenye mashamba.