1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Luteka za pamoja kati ya Japan, Marekani na Korea ya Kusini

Oumilkheir Hamidou
10 Desemba 2017

Japan itafanya luteka za kijeshi pamoja na Marekani na Korea ya Kusini wiki hii kwa lengo la kufanya majaribio ya makombora ya kuchunguza hujuma za angani.

US-Stützpunkt Humphreys in Südkorea
Picha: picture-alliance/Yonhapnews Agency

Habari hizo zimetangazwa na viongozi wa serikali mnamo wakati ambapo vitisho vya usalama vinazidi kuongezeka kutoka Korea ya Kaskazini.

Tangazo la luteka za pamoja, za sita za aina hiyo tangu mwaka 2016 limetolewa  wiki karibu mbili baada ya viongozi wa mjini Pyongyang kufyetua kombora la nuklea linaloweza kushambulia toka bara moja hadi jengine, kuelekea baharini, ndani ya kanda ya kiuchumi ya Japan, mwishoni mwa mwezi uliopita.

Luteka hizo za pamoja kati ya Japan, Marekani na Korea ya Kusini zitafanyika karibu na pwani ya Japan kesho jumatatu na jumanne, amesema hayo waziri wa ulinzi Itsunori Onodera alipokuwa anakitembelea kikosi cha Japan kaskazini mwa nchi hiyo.

Ndege ya kivita ya Marekani chapa F-22Picha: picture-alliance/Yonhap

Japan, Marekani na Korea ya Kusini kusaka njia za kinga dhidi ya makombora ya Korea ya Kaskazini

Luteka hizo zimelengwa "kufanya mazoezi ya kufuatilizia chombo na kupashana habari miongoni mwa nchin hizo tatu kuhusu chombo hicho"-amesema afisa mmoja wa ulinzi ambae hakutaka jina lake litajwe.

"Zoezi hilo litapelekea kuibuka mkakati dhidi ya makombora yenye uwezo wa kushambulia bara moja hadi jengine," afisa huyo wa ulinzi amesema.

Mivutano kuhusu miradi ya silaha za nuklea za Korea ya kaskazini imezidi makali mwaka huu, huku Pyongyang ikifanya jaribio lake la sita la silaha hizo sawa na kufyetua makombora kadhaa , na kupuuza vikwazo kadhaa vilivyowekwa na Umoja wa mataifa.

Mwakilishi maalum wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Korea ya kaskazini atakwenda Japan na Thailand wiki hii kwa mazungumzo yanayohusiana na juhudi za kuzidisha shinikizo dhidi ya Pyongyang baada ya jaribio lake la hivi karibuni la kombora lenye uwezo wa kushambulio toka bara moja hadi jengine.

"Marekani imedhamiria kuendeleza ushirikiano wake pamoja na nchi zote hizo mbili kwa namna ambayo Korea ya kaskazini itarejea katika meza ya mazungumzo kuhusu namna ya kuachana na silaha za nuklea"taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema.

Kiongozi wa Korea ya kaskazini Kim Jong UnPicha: picture alliance/AP Photo/Korean Central News Agency

Onyo dhidi ya uamuzi mbaya kuhusiana na mradi wa nuklea wa Korea ya kaskazini

Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameonya jana jumamosi dhidi ya hatari inayoweza kusababishwa na uamuzi mbaya katika ugonvi pamoja na Korea ya kaskazini na kuwahimiza viongozi wa Pyongyang waache wazi njia za mawasiliano, baada ya ziara adimu kufanyika katika nchi hiyo iliyotengwa na dunia.

Ziara ya Jeffrey Feltman Korea ya kaskazini, ya kwanza ya aina yake kuwahi kufanywa na mwanadiplomasia wa umoja wa mataifa tangu mwaka 2010, imetokea baada ya Marekani na Korea ya Kusini kuanzisha luteka zao za pamoja za angani, kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa.

Korea ya kaskazini imesema kwa mara nyengine tena inaziangalia luteka hizo kuwa ni za uchokozi na kwamba zimelengwa kuandaa hujuma za kinuklea dhidi yake.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri        Isaac Gamba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW