LUXEMBOURG: Rais Mugabe hatoalikwa mkutano wa Novemba
19 Juni 2007Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ureno,Luis Amado amesema,Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe hatoalikwa kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika,unaotarajiwa kufanywa mwezi Novemba katika mji mkuu wa Ureno, Lisbon. Waziri huyo,amenukuliwa akisema kwamba hana hamu ya kumuona Mugabe mjini Lisbon kwa sababu atakuwa chanzo cha matatizo.Rais Mugabe na zaidi ya maafisa 100 wa Zimbabwe walio karibu na utawala wake,wamewekewa vikwazo vya usafiri katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Mugabe kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais mwaka 2002.Watazamaji wa kimataifa walisema,uchaguzi huo ulikuwa wa udanganyifu na visa vya kuandama na kukandamiza wapinzani.Baadhi ya viongozi mashuhuri barani Afrika,wamepinga hatua yo yote ya kumzuia Rais Mugabe kuhudhuria mkutano huo wa kilele kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya.