1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 wakaidi amri ya kusitisha mapigano Kongo

8 Machi 2023

Waasi wa M23 wamepambana na mashambulizi kutoka pande mbili mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo licha ya makubaliano ya kikanda ya kusitisha mapigano yaliyopangwa kutekelezwa siku hiyo hiyo.

Demokratische Republik Kongo | Soldaten der EACRF und M23 Rebellen in Kibumba
Picha: GLODY MURHABAZI/AFP/Getty Images

Baada ya siku kadhaa za utulivu, mapigano yalizuka Jumatatu katika jimbo la Kivu Kaskazini, na kusababisha raia kadhaa kuuawa na kujeruhiwa kwa mujibu wa vyanzo vya hospitali na wafanyikazi wa misaada.

SOMA PIA; Waasi wa M23 wakabiliana na jeshi la Kongo

Mapigano hayo yaliendelea siku ya Jumanne, huku waasi wakiteka vijiji vipya, licha ya usitishaji mapigano uliosimamiwa na Angola wiki iliyopita ambao ulipaswa kuanza saa sita mchana.

Waasi wa M23 wameteka maeneo mengi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu walipoibuka tena kutoka kwenye makazi yao mwishoni mwa 2021, wakidai kuwa serikali ilipuuza ahadi ya kuwajumuisha katika jeshi.

Kundi linaloongozwa na Watutsi limekizingira kitovu cha biashara cha Goma kando ya ziwa, na kuchukua eneo la kaskazini mwa jiji na kusonga mbele upande wa magharibi.

Mapigano hayo mapya yalienda sambamba na ombi la dharura la mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres la kuwataka waasi wa M23 kuheshimu usitishaji mapigano na kujiondoa kikamilifu katika nchi hiyo yenye migogoro.

SOMA PIA; Mzozo wa Kongo wajadiliwa Bujumbura

M23 katika taarifa yao walitangaza kile walichokiita "usitishaji vita unaofaa ili kufungua njia ya mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Kinshasa".

Duru mpya ya mapigano

Picha: Alexis Huguet/AFP

Pande zote mbili zinashutumia kwa kuanzisha duru mpya ya mapigano. Msemaji wa M23 Willy Ngoma aliambia AFP kwamba kundi hilo lilikuwa likijilinda baada ya jeshi kushambulia maeneo yake yote kwa wakati mmoja.

Kwa upande  mwengine msemaji wa jeshi wa Kivu Kaskazini Luteni Kanali Guillaume Ndjike, alisema kwamba M23 "na wafadhili wao kutoka Jeshi la Ulinzi la Rwanda" walishambulia kikosi cha Burundi kilichotumwa ambacho ni sehemu ya kikosi cha kijeshi la kikanda cha Afrika Mashariki.

Aidha Luteni Kanali Ndjike amesema mashambulizi ya waasi pia yalilenga kambi ya wakimbizi na eneo la Mubambiro, kilomita 20 magharibi mwa Goma, na kusababisha "uharibifu mkubwa".

 Kongo inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi, ambao wamesababisha zaidi ya watu nusu milioni kuyakimbia makaazi yao.

Wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa, Marekani, pamoja na mataifa kadhaa ya magharibi, wanakubaliana na tathmini hiyo, ingawa Rwanda inakanusha vikali.

Mnamo Machi 3, ofisi ya rais wa Angola ambayo ni mpatanishi wa mzozo huo ilitangaza kusitisha mapigano mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuanza kutekelezwa Jumannne saa sita mchana.

 

//AFP, dpa

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW