1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 waukamata tena mji wa Kalembe mashariki ya Kongo

24 Oktoba 2024

Mji wa Kalembe, ambao ni muhimu kuelekea kwenye machimbo ya madini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulianguka tena mikononi mwa kundi la wapiganaji wa M23 tangu mchana wa Jumatano.

DR Kongo | Soldaten in Kirumba
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Vyanzo vya ndani vimeeleza kuwa wanamgambo wa M23 wameuchukuwa mji huo baada ya mapigano makali baina yao na makundi ya vijana wanaojiita wazalendo ambao baada ya kuzidiwa walikimbilia mji wa Pinga ulio umbali wa takribani kilomita 35 na mji huo wa Kalembe uliotwaliwa na M23. Asubuhi Alhamisi wapiganaji wa kundi hilo wameonekana wakishika doria kwenye mji huo muhimu wilayani Walikale vimeeleza vya ndani. Benjamin KASEMBE na mengi zaidi kutoka Goma.))

Vyanzo vya ndani vinadai kuwa baada ya mapigano ya takribani masaa matatu, wapiganaji wa kundi la M23 walifanikiwa kuuteka mji wa Kalembe, huku milio ya risasi ikiendelea kurindima hadi jioni ya Jumatatu.

Soma pia: Makubaliano ya kusitisha mapigano DRC yavunjika

Waasi wa M23 wanaendesha harakati zao mashariki ya Kongo wakisaidiwa na RwandaPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Mashahidi wanasema wanamgambo wengine kundi hilo walijikita katika kijiji kidogo cha Ihula wakizidi kuusogelea mji mwingine wa Pinga wilayani Walikale ambako hali ya wasiwasi imezidi kuongezeka na raia wakikimbia kuelekea mji mkuu wa wilaya hiyo.

DW imezungumza na raia mmoja wa Kalembe ambaye hakutaka jina lake litajwe:

"Mimi nilitoka kalembe hiyo jana wakati wa mapigano hayo baina ya Wazalendo na M23. Raia wote tulilazimika kukimbilia kwenye kituo cha afya, lakini mabomu yalikuwa yakirushwa kiholela kote mjini. Ninachofahamu ni kuwa watu wawili walijeruhiwa lakini hakuna aliyefariki katika mapigano hayo ." Amesema raia mmoja wa Kalembe.

Kuanguka kwa mji huu muhimu wa Kalembe ni pigo kubwa kwa serikali ya Kongo ambayo hadi sasa inasema inaendelea kuheshimu mkataba wa usitishwaji mapigano kama ilivyotakiwa na mpatanishi wa mzozo huu, Angola. Kihangi PRINCE ni raia na mbunge wa zamani mzaliwa wa Walikale akieleza hofu yake.

Soma pia: Waasi wa M23 waudhibiti mji muhimu wa Kalembe wilayani Masisi

"Mtaa wa Walikale ni eneo tajiri lenye madini. Kuna kiwanda kikubwa cha madini. Iwapo adui watapata nguvu nyingi sana, kiwanja kidogo cha ndege kilicho hapo kitawasaidia saaa kusonga mbele."

Mwaka wa 2023, waasi wa M23 walikamata barabara inayounganisha Goma na Minova-BukavuPicha: ALEXIS HUGUET/AFP

Upande mwingine katika wilaya jirani ya Masisi, waasi wa M23  walishambulia kijiji cha Kahira kilichokuwa  chini ya udhibiti wa vikosi vya wapiganaji wanaojiita Wazalendo waliozidiwa nguvu mbele ya M23.

Wakizungumza na DW, raia wa mji wa Goma wamesema wameanza kupoteza matuamaini ya upatikanaji wa amani kufuatia kusonga mbele kwa M23: "Tunataka serikali itueleweshe maana ya  vita hivi, sababu kama raia tunasumbuka sana. Uchumi wetu umeathirika pakubwa ".   , "kwa nini jeshi letu halipigani na M23 japokuwa wao wanasonga mbele ".

Tangu Jumapili wiki hii, mapigano makali yamekuwa yakishuhudiwa kati ya waasi wa M23 na makundi yanayojihami kwa silaha maarufu kama Wazalendo kwenye mji huo wa Kalembe. Katika mapigano ya Jumatatu, jeshi la Kongo  lilitumia helikopta kuwatawanya M23 kuwasaidia washirika wake lakini bila mafanikio.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW