1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

M23 yaendelea kuwepo Walikale licha ya kutangaza kujiondoa

24 Machi 2025

Kundi la waasi wa M23 limeendelea kushikilia mji muhimu wa Walikale, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, licha ya awali kutangaza mpango wa kuondoka ili kutoa nafasi kwa mazungumzo ya amani.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Goma 2012 | Waasi wa M23 wajiondoa mjini
Waasi wa M23 wamechukuwa udhibiti wa maeneo makubwa Kongo MasharikiPicha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Kundi linaloungwa mkono na Rwanda la M23 lilitangaza Jumamosi kuwa limeanza kuondoa vikosi vyake nje kidogo ya mji wa Walikale ili kuweka mazingira mazuri ya "amani na mazungumzo ya kisiasa." Hata hivyo, kundi hilo lilisema halitaruhusu jeshi la serikali kurejea katika mji huo wenye wakazi takriban elfu 60, likionya kuwa shambulizi au uchokozi wowote utafuta moja kwa moja uamuzi wao.

Wanajeshi wa serikali ya Kongo walisema Jumamosi jioni kuwa watafuatilia kwa umakini uondoaji huo wa M23 na hawatachukua hatua yoyote ya kijeshi, wakiwataka wanamgambo wanaoiunga mkono serikali wafanye hivyo pia ili kupunguza mvutano. Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Kayikwamba, alisema wanatazama kuona ikiwa kweli M23 itaondoka na kuipa kipaumbele njia ya mazungumzo.

Soma pia:Waasi wa M23 wauteka mji wa Walikale licha ya juhudi za amani 

Nani ananufaika na machafuko ya Kongo?

03:05

This browser does not support the video element.

Siku ya Jumapili, wakazi na duru za kijeshi mjini Walikale waliripoti kuwa hapakuwa na mapigano yoyote katika eneo hilo lililokuwa likishambuliwa vikali hivi karibuni na ndege za jeshi la Kongo. Mkazi mmoja alisema walipoamka hali ilikuwa tulivu, na M23 bado walikuwa mjini humo. Hata hivyo, mapigano yaliripotiwa kati ya M23 na wanamgambo wa Wazalendo wanaounga mkono serikali katika mkoa jirani wa Kivu Kusini.

Awali, wawakilishi wa serikali na M23 walipanga kukutana tarehe 18 Machi mjini Luanda, Angola, lakini mazungumzo hayo yalifutwa dakika za mwisho. Hata hivyo, Rais wa DRC Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, walikutana ghafla mjini Doha chini ya uratibu wa Qatar, ambapo waliahidi tena nia yao ya kutekeleza usitishaji mapigano mara moja. Lakini licha ya jitihada hizo za kidiplomasia, mapigano bado yanaendelea katika maeneo mbalimbali mashariki mwa Kongo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW