1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 yatangaza kujiondoa vijiji ilivyoviteka Congo

11 Aprili 2022

Waasi wa kundi la M23 wametangaza Jumapili kuondoka kutoka vijiji walivyoviteka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wiki iliyopita, kufuatia makabiliano na vikosi vya serikali katika wilaya ya Rutshuru.

Demokratische Republik Kongo | Soldaten nach Kämpfen mit Rebellengruppe M23
Picha: Guerchom Ndebo/AFP/Getty Images

Mapigano kati ya waasi hao na wanajeshi yalipamaba moto siku ya Jumatano baada ya siku kadhaa za utulivu na waasi wa M23 kuchukuwa udhibiti wa vijiji kadhaa vya eneo la Rutshuru katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Kundi hilo limesema M23 ilifanya uamuzi wa kujiondoa mara moja kwenye maeneo mapya iliyoyadhibiti ili kutoa nafasi ya kushughulikia masuala yake kupitia majadiliano na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Wanajeshi wa DRC wakifanya doria mitaa ya Rutshuru katika magari yao siku chache baada ya makabiliano na waasi wa M23 mjini Rutshuru.Picha: Guerchom Ndebo/AFP/Getty Images

Soma pia: Mapigano yazuka baina ya jeshi la Kongo na waasi wa M23

Taarifa ya kundi hilo imesema M23 haikuwa na nia ya kuteka maeneo ili kuyaendesha, na kuongeza kuwa dhamira yao ni kufikia suluhisho la amani la mzozo huo. Lakini haikuthibitishwa kufikia Jumapili mchana, iwapo uondokaji huo kutoka dazeni kadhaa za vijiji ulifanyika kweli.

Waasi wa M23 walikuwa wamevikalia vijiji vya Gisiza, Gasiza, Bugusa, Bikende-Bugusa, Kinyamahura, Rwambeho, Tshengerero, Rubavu na Basare, na waliendelea kudhibiti vijiji vya Runyoni na Tchanzu, kwa mujibu wa msemaji wake katika vijiji vilivyoko karibu na Jomba.

Soma pia: Raia 13,000 waingia Uganda wakikimbia mapigano ya M23

M23 ilisema pia kuwa inalenga kukabidhi wanajeshi wote wa jeshi la taifa waliotekwa kwenye uwanja wa mapambano kwa shirika la kimataifa la Msalaba mwekundu kwa ajili ya kuhudumiwa ipasavyo.

Asili ya M23

Kundi la M23 lilianzishwa na wanachama wa zamani wa kundi la wanamgambo wa Kitutsi ambao walikuwa wanaungwa mkono na Rwanda na Uganda. Waasi hao walikuwa wamejumuishwa katika jeshi la Congo chini ya makubaliano yaliosainiwa Machi 23, 2009.

Mkuu wa M23, Roger Lumbala akisaini nyaraka Februari 6, 2013 mjini Kampala, wakati wa mazungumzo ya amani na serikali ya Congo baada ya kuuteka kwa muda mji wa Goma.Picha: Isaac Kasamani/AFP/Getty Images

Mnamo mwaka 2012, waliasi, wakisema makubaliano hayo hayakuheshimiwa na kuliita kundi lao Vuguvugu la Machi 23, yaani M23.

Soma pia: DRC yaituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23

Likiwa moja ya makundi kadhaa ya silaha yanayorandaranda mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kundi la M23 liliuteka kwa muda mfupi mji wa Goma kabla ya kushindwa na kulaazimishwa kuondoka nchini humo.

Baada ya kushindwa kwao, hatimaye M23 ilisaini makubaliano na serikali ya Kinshasa ambayo yalijumuisha vipengele juu ya kuingizwa kwa wapiganaji wao katika jamii ya kiraia.

Soma pia:Uganda yawakamata wapiganaji 40 wa M23

Lakini kundi hilo limishtumu tena serikali kwa kukiuka makubaliano hayo na kurejea kupigana mwaka uliopita. Mashambulizi yao ya mwisho yalianza mwishoni mwa mwezi Machi.

Chanzo: AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW