Maaambukizi ya virusi vya corona Afrika yapindukia milioni 2
19 Novemba 2020Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vimetoa taarifa leo Alhamisi kwamba idadi ya maaambukizi ya virusi vya corona barani humo imepindukia milioni 2 na hivyo kuanza kuingia katika wimbi la pili la maambukizi.Bara la Afrika lenye jumla ya nchi 54 pia limeshuhudia zaidi ya vifo vya watu 48,000 kutokana na ugonjwa wa COVID-19. Mkurugenzi wa Afrika wa taasisi ya kuzuia magonjwa CDC John Nkengasong ameelezea wasiwasi wake kuhusiana na kushuka kwa kiwango cha uvaaji wa barakoa barani humo. Nchi kadhaa za Afrika zimethibitisha kuongezeka kwa maambukizi ya corona. Afrika Kusini inaongoza kwa zaidi ya watu 750,000, walioambukizwa ikifuatiwa na Morocco, Misri na Ethiopia. Kenya katika siku za hivi karibuni imeshuhudia kuongezeka kwa maambukizi miongoni mwa raia wake.