Maadhimisho ya siku ya kuienzi Dunia
22 Aprili 2021Hata hivyo, taasisi na mashirika mbalimbali yameridhia wito wa serikali wa kuongeza kiasi cha misitu kwa asilimia 10 kupitia upandaji wa miti.
Wadau mbalimbali wamekongamana hii leo kwa zoezi la upandaji miti, kuandimishi siku ya ardhi ulimwenguni. Serikali ya Kenya imesisitiza juhudi zake za kuhakikisha ongezeko la misitu kwa asilimia 10 kufikia mwaka 2030, kama njia moja ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Dunia yahitaji hatua thabiti kulinda mazingira
Wakenya wanakabiliwa na tishio la majanga mawili tofauti yanayotokea wakati mmoja yakisababisha ukosefu wa chakula. Magharibi mwa Kenya, sehemu zinazopakana na Ziwa Victoria pamoja na baadhi ya maeneo ya bonde la ufa, yakiripotiwa kushuhudia mafuriko, nazo kaunti za Turkana, Mandera na Marsabit, pamoja na kaunti zingine sita zikishuhudia ukame.
Viwango vya juu zaidi vya joto ulimwenguni
Wimbi la pili la nzige wa jangwani vilevile liliripotiwa kuvamia kaunti 15 nchini ikiwemo Nakuru, Meru na Laikipia ambayo ni maeneo yanayotambulika kwa kiwango kikubwa cha uzalishaji wa chakula. Isitoshe taifa linapambana na janga la kiafya la ugonjwa wa COVID 19 ambao ni tishio kubwa kwa afya ya watu na mazingira yetu.
Mtaalam wa maswala ya mazingira Jackson Kinyanjui kutoka shirika la Climate Change Kenya ameeleza kuwa katika kipindi cha kati ya mwaka 2010 hadi 2020, asasi ya kimataifa inayoshughulikia maswala ya mabadiliko ya tabia nchi, imerekodi mara kumi viwango vya juu zaidi vyajoto ulimwenguni.
"Madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi yana uhusiano mkubwa na joto ambalo tumekuwa tukilishuhudia ulimwenguni. Hii ni changamoto kwa serikali kuweka mikakati katika miundo mbinu yao yote ili kuthibiti hali,” amesema Kinyanjui.
Wito wa kuimarisha mikakati ya uzalishaji chakula
Idadi ya watu nchini inakadiriwa kuendelea kuongezeka, na hii inamaanisha, watu zaidi wanaohitaji lishe. Usalama wa wananchi hutishiwa pale kunapokuwa na ukosefu wa chakula cha kutosha. Shirika la Yara East Africa linalohudumu eneo la Afrika Mashariki ni kati ya wadau wa maswala ya kilimo wanaowafikia wakulima katika maeneo yanayoshiriki kilimo kwa kiwango kikubwa nchini, ili kuboresha uzalishaji wa chakula.
"Tunalenga kuimarisha uwezo wa wakulima kuboresha mazao yao. Hii ni kupitia mafunzo ya mbinu za kilimo. Kwa muda mrefu tumezingatia ubora wa pembejeo lakini sasa, tunahimiza upimaji wa mchanga wa mashamba ya kila mkulima kwa bei nafuu,” amesema Vitalis Wafula, Meneja mkuu wa mauzo katika shirika la Yara East Africa.
Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusu mazingira, UNEP, kimebuni mfumo unaotoa data inayoonyesha namna kila taifa linachangia malengo ya mabadiliko kwenye tabia nchini ya mkataba wa Paris wa mwaka 2015, uliotiwa saini na zaidi ya mataifa 190.