1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani

8 Machi 2012

Haki ya wanawake kushiriki katika maisha ya kisiasa imesisitizwa katika mikataba kadhaa ya kimataifa, lakini kuibadilisha haki kutoka kwa maandiko hadi kwenye vitendo kunahitaji jitihada zaidi miongoni mwa wahusika.

Liberian President Ellen Johnson-Sirleaf stands at a ceremony to mark her second presidential inauguration at the Capitol in Monrovia January 16, 2012. Johnson-Sirleaf is Africa's first woman president. REUTERS/Larry Downing (LIBERIA - Tags: POLITICS)
Rais Ellen Johnson-Sirleaf wa Liberia EllenPicha: Reuters

Kulingana na ripoti mpya ya utafiti iliyochapishwa kwa ushirikiano wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa – UNDP na Taasisi ya Taifa ya Demokrasia kwa Masuala ya Kimataifa, ni kwamba ijapokuwa asilimia 40 hadi 50 ya wanachama wa vyama vya kisasa kote ulimwenguni ni wanawake, asilimia 10 pekee ndio inashikilia nyadhifa za uongozi.

Msimamizi wa UNDP Helen Clark anasema kuwa huku kukiwa na chini ya asilimia 20 ya viti vya bunge ulimwenguni vinavyokaliwa na wanawake, ni wazi kwamba vyama vya kisiasa vinahitaji kupiga hatua zaidi na vinahitaji kusaidiwa katika juhudi hizo, za kuwasaidia wanawake katika kujiimarisha kisiasa.

Ushiriki wa vyama vya siasa ni muhimu kwa wanawake

Mkurugenzi wa Kikundi cha Jinsia cha Shirika la UNDP Winnie Byanyima ameliambia shirika la habari la IPS kuwa ikiwa tunataka kueneza demokrasia na kuwapa uwezo wanawake kisiasa, ni sharti tushirikiane na vyama vya kisiasa. Byanyima ambaye ni mbunge wa zamani wa Uganda na pia mwanadiplomasia aliongeza kuwa Ikiwa wanawake hawapewa uongozi wa vyama vya kisiasa, basi hawawezi kuziongoza serikali. 

Naibu Katibu Mkuu wa UN Asha-Rose Migiro,Picha: AP

Kimataifa, idadi ya mawaziri wanawake serikalini iko chini ikiwa ni kiwango cha wastani cha asilimia 16. Na idadi ya viongozi wanawake  wa nchi na serikali bado iko chini, na imepungua katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa nini chini ya asilimia tano katika mwaka wa 2011.

Utafiti huo unasema idadi hiyo ya chini imeendelea kushuhudiwa katika miongo mitatu iliyopita ya uhamasisho na juhudi za jamii ya kimataifa kuangamiza ubaguzi na kuwapa uwezo wanawake.

Umoja wa Mataifa watambua jukumu la wanawake

Na hili linafanyika licha ya ukweli kuwa Umoja wa Mataifa ulilitambua jukumu muhimu la wanawake katika maendeleo ikiwemo kuwapa uwezo wanawake kama mojawapo ya malengo manane ya Maendeleo ya Milenia katika mwaka wa 2000. Lakini kwa mujibu wa utafiti huo, hakuna eneo lolote ulimwenguni ambalo liko katika harakati za kufikia asilimia 30 ya wanawake katika nafasi za kufanya maamuzi.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary ClintonPicha: dapd

Ijapokuwa kunayo maeneo yanayojaribu kujizatiti na kutimiza lengo hilo, vizingiti kadhaa vingali njiani mwa juhudi za wanawake kushiriki kikamilifu kama wagombea.

Kulingana na takwimu za hivi punde za Chama cha Kimataifa cha Wabunge IPU na Wanawake wa Umoja wa Mataifa, idadi ya wanawake kama viongozi wa nchi au serikali ni 18 kati ya nchi 193.

Utafiti huo wa UNDP na NDI unataja baadhi ya mikakati inayoweza kutumiwa wakati wa uchaguzi, kama vile kuwapa mafunzo na kuwahimiza wagombea wa kike na kuhakikisha wanawake wanaonekana kwa wingi katika kampeni.

Wanawake na wanaume wawe katika uwiano sawa kimaendeleo

Shirika la NDI linasema limefanya kazi na zaidi ya vyama 720 vya kisiasa na mashirika katika zaidi ya nchi 80 ili kuweka mazingira bora na ya wazi ambapo wanaume na wanawake wanaweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa demokrasia.

Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu Navi PillayPicha: AP

Katika awamu ya kabla ya uchaguzi, usajili na uteuzi wa wagombea ni shughuli muhimu zaidi ya kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki siasa. Lakini pengo la jinsia hupanuka kwa kiwango kikubwa wakati wagombea wa nyadhifa za kisiasa wakisonga kutoka hatua ya kuwa halali na kuwa wagombea, na kisha kuteuliwa na chama kuwa wagombea wa nyadhifa hizo.

Utafiti huo unataja mifano kadhaa ya usawa wa kijinsia chama kimoja cha kisiasa nchini Canada kina kamati ya kuwasajili wagombea ili kuhakikisha mchanganyiko katika uteuzi wa wagombea. Nchini Costa Rica, moja ya vyama vya kisiasa hubadilisha wagombea wa kiume na kike kwenye orodha ya uchaguzi.

Nchini Afrika Kusini, wanachama wa kike katika vyama walishinikiza mabadiliko katika ratiba ya bunge ili kuwajumuisha wabunge wenye familia, na pia wakashinikiza mijadala kumalizika mapema jioni ili kuwapa nafasi wabunge walio na familia na kwa vifaa vya malezi ya watoto kuwekwa.

Nchini Ujerumani, chama cha Christian Democratic Union (CDU) kiliidhinisha asilimia 33 ya viti maalum vya maafisa wa chama katika mwaka wa 1996. Na ikiwa viti hivyo maalum havitapatikana, uchaguzi wa ndani sharti urudiwe.

Mwandishi: Bruce Amani/IPS
Mhariri: Josephat Charo