1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafa ikiwa Rais Saleh wa Yemen atarejea nyumbani

10 Juni 2011

Bado sio hakika kama Ali Abdullah Saleh atakuwa mtawala wa tatu wa Kiarabu kufyekwa kutoka madarakani kutokana na wimbi la mapinduzi ya Kiarabu.

Rais wa Yemen Ali Abdullah SalehPicha: dapd

Rais huyo wa Yemen wa muda mrefu sasa tayari ameshatangaza kwamba atarejea nchini mwake kutoka Saudi Arabia. Mtu anaweza tu kuufahamu uamuzi huo kuwa ni kama tishio.

Kinyume na ilivyotokea Misri na Tunisia, mtawala huyo alilazimika aondoke nchini kwa sababu ya kujeruhiwa na shambulio la roketi. Hata hivyo, hiyo sio ishara nzuri kwa mustakbali wa Yemen.

Wanajeshi wa Yemen waungana na waandamanaji wanaoipinga serikali.Picha: picture-alliance/dpa

Kurejea kwa Ali Abdullah Saleh huko Yemen kutakuwa ni maafa, ni kama kuwapiga vibao waandamanaji wengi walio vijana ambao kwa miezi sasa wamekuwa wakienda mabarabarani kutaka kuwa na mustakbali wa kidimokrasia kwa nchi yao. Vijana hao hadi sasa wamekuwa hawataki nchi yao iingie katika malumbano ya umwagaji damu baina ya jeshi na wapiganaji wa kikabila. Pindi mtawala huyo atarejea nchini , basi nchi hiyo inaweza bila ya wasiwasi ikaangukia katika vita vya kienyeji na baadae dola kusambaratika. Matokeo yake ni kwamba huenda kutakuweko pengo la usalama lililo la hatari. Watakaofaidika, kwa mujibu wa mtizamo wa Ali Abdullah Saleh, ni zile nguvu zozote ambazo ni washirika wa wale wanaopigana dhidi ya nchi za Magharibi na pia Saudi Arabia: nao ni mtandao wa kigaidi wa al-Qaida.

Jamii ya kimataifa isikubali kuzibwa macho yake na hoja hiyo, na inafaa waziwazi jamii hiyo ya kimataifa imtake Ali Abdullah Saleh asirejee nyumbani, na kwamba rais huyo awache njia wazi ya kuteuliwa baraza la utawala la kujishikiza. Tangu hapo Saudi Arabia, katika muktdhaa huu, ina wajibu, na tayari zamani imestayarisha mpango wa kutekelezwa. Saudi Arabia, jirani mwenye nguvu na aliye tajiri, ina ufunguo katika utatuzi wa suala la Yemen. Kwa miongo ya miaka watawala wa Saudi Arabia wameshirikiana na Ali Abdullah Saleh, lakini nchi hiyo pia ina mawasiliano mazuri na wapinzani wakubwa wa Ali Abdullah Saleh ndani ya makabila na ndani ya jeshi.

Rais Ali Abdullah Saleh (kushoto) akipeana mkono na Mfalme Abdullah al-Aziz wa Saudi Arabia.Picha: ap

Lakini mchango wa Saudi Arabia lazima pia uangaliwe kwa mtizamo wa kihakiki. Utawala wa kifalme wa Riyadh hauna hamu hata kidogo kuona majaribio ya kidimokrasi yanafaulu katika eneo la Bara Arabu. Huko Bahrain imesaidia, kijeshi, kulitia kabari vuguvugu la kidimokrasia katika nchi hiyo. Huko Yemen, Saudi Arabia itaweza kujaribu kushikilia kwamba kipindi cha mpito wawemo ndani ya utawala watu wa makabila wenye siasa za kiasilia pamoja na wakuu wa kijesdhi, hivyo kulazimisha kukaa pembeni nguvu za kimapinduzi. Watu waliokwenda katika mabarabara ya Sanaa na Taiz katika mnamo wiki zilizopita hawajapigania kuweko mfumo wa kisasa wa utawala wa kikabila, lakini watu hao wamepigania kuweko demokrasia, watu wote wakishiriki ndani ya demokrasia hiyo .

Mwandishi : Sollich, Rainer/ Miraji Othman/ZR

Mhariri: Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW