1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa 200 wa polisi ya Kenya wawasili Haiti

Josephat Charo
17 Julai 2024

Maafisa wengine 200 wa polisi ya Kenya wamewasili nchini Hati, chini ya mwavuli wa tume inayoungwa mkono na Umoja wa Matafa, kujaribu kutuliza machafuko ya mara kwa mara yanayofanywa na magenge yaliyojihami na silaha.

Maafisa wa kikosi cha kwanza cha polisi wa Kenya baada ya kutua uwanja wa ndege wa Toussaint Louverture.
Maafisa wa kikosi cha kwanza cha polisi wa Kenya baada ya kutua uwanja wa ndege wa Toussaint Louverture.Picha: Marckinson Pierre/dpa/AP/picture alliance

Duru nchini Haiti zinaelezwa kuwa maafisa wa polisi kutoka Kenya wamekaribishwa na maafisa wa vyeo vya juu wa Haiti pamoja na maafisa wengine kutoka Kenya walio huko Haiti.

Mkurugenzi Mkuu wa polisi ya Haiti Rameau Normil amewakaribisha maafisa wa Kenya akiwa ameandamana na kamanda wa kikosi cha kwanza cha Kenya, kilichopo Haiti, Godfrey Otunge. Huyu hapa Normil.

"Asubuhi hii kikosi cha pili cha maafisa wa polisi wa Kenya, ambao ni sehemu ya ujumbe wa kikosi cha ulinzi cha kimataifa kuisaidia polisi ya kitaifa ya Haiti kupambana na magenge yenye silaha nchini, kimewasili. Kwa niaba ya serikali, na baraza la raisi, nawakaribisha nchini Haiti."

Duru nchini Haiti pia zinasema idadi ya maafisa wa polisi kutoka Kenya sasa imefikia 400 katika mji mkuu Port-au-Prince unaokabiliwa na machafuko, ikiwa ni sehemu ya juhudi zinazofuatiliwa kwa karibu sana kupeleka maafisa 1,000 kusaidia kuleta uthabiti nchini Haiti.

Kwa upande wake Godfrey Otunge, naibu jenerali wa polisi na kamanda wa kikosi cha Kenya nchini Haiti alisema, "Tunategemea msaada wenu. Polisi ya taifa la Haiti tayari inafanya kazi na kikosi cha kwanza cha polisi wa Kenya na tunaendelea kupata matunda ya juhudi zetu za pamoja zinazolenga kuiwezesha Haiti kurejesha tena uthabiti na kuwa dola imara kiuchumi."

Duru za polisi nchini Kenya zinasema kufikia sasa maafisa 600 wameondoka kwenda Haiti, wakiwemo wale waliowasili siku ya Jumanne. Chanzo kimoja kimeliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba maafisa zaidi wa polisi wataondoka Nairobi hivi karibuni mpaka idadi ya maafisa 1000 ikamilike.

Kikosi cha polisi kutoka Kenya ni sehemu ya kikosi cha tume ya kimataifa ambacho kimepata vipingamizi vya kisheria mjini Nairobi, ambako rais wa Kenya William Ruto anajaribu kutuliza maandamano ya kuipinga serikali yake.

Taifa hilo la Afrika Mashariki linaongoza kikosi kinachotarajiwa kuwajumuisha maafisa 2,500. Nchi nyingine, nyingi za bara la Afrika na eneo la Karibik, pia zinachangia maafisa wao katika tume hiyo, ambayo imepata ridhaa ya Umoja wa Mataifa, ingawa haisimamiwi na umoja huo.

Kikosi cha Haiti chapingwa Kenya

Tume ya kimataifa nchini Haiti iliridhiwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Oktoba mwaka uliopita, lakini ikacheleweshwa na uamuzi wa mahakama ya Kenya mnamo mwezi wa Januari mwaka huu iliyotoa hukumu kwamba tume hiyo ilikuwa kinyume na katiba. Mahakama ilisema utawala wa rais Ruto haukuwa na mamlaka ya kuwapeleka maafisa wake nje ya nchi bila makubaliano ya pamoja.

Serikali ya Kenya ilifikia makubaliano na Haiti mwezi Machi, lakini chama kidogo cha upinzani cha Third Alliance, kimewasilisha shauri mahakamani katika juhudi nyingine ya kuizuia tume ya Haiti.

Soma pia: Kiksoi cha pili cha ujumbe wa polisi kuwasili Haiti

Marekani ilikuwa ikitafuta kwa bidii nchi ya kuiongoza tume hiyo ya Haiti na inatoa msaada wa fedha na uratibu. Rais wa Marekani Joe Biden alifutilia mbali wazi wazi kuwapeleka wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya Haiti, taifa masikini kabisa katika eneo la Amerika, ambako Marekani ina historia ya kuingilia kati kusuluhisha mizozo.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, limeelezea wasiwasi wake kuhusu tume ya Haiti na mashaka kuhusu ufadhili, huku mashirika mengine mara kwa mara yakiituhumu polisi ya Kenya kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kufanya mauaji kinyume na sheria.

Haiti kwa muda mrefu imekabiliwa na machafuko yanayofanywa na magenge ya wahalifu, lakini hali ilibadilika ghafla kuwa mbaya mwishoni mwa mwezi Februari wakati magenge yaliyojihami na silaha yalipoanzisha mashambulizi ya kupanga mjini Port-au-Prince, yakisema yalitaka kumpindua waziri mkuu wa wakati huo, Ariel Henry.

Machafuko mjini Port-au-Prince yameathiri usalama wa upatikanaji wa chakula na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, huku sehemu kubwa ya mji huo mkuu ikiwa mikononi mwa magenge yanayotuhumiwa kwa ukiukaji wa haki yakiwemo mauaji, ubakaji, uporaji na utekaji nyara.

(afp)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW