Maafisa Uganda wapendekeza sheria ya chanjo kuwa lazima
8 Februari 2022Muswaada huo unalenga kuwatia shime watu zaidi kujitokeza kuchomwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Muswaada huo wa sheria ambao unaweza bado kufanyiwa marekebisho unakabiliwa na uwezekano wa kufanyiwa tathmini ya kina na kamati ya bunge inayohusika na masuala ya afya.
Aidha sheria hiyo inayopendekezwa inatowa mwito wa mtu kuchukuliwa hatua ya kufungwa jela hadi miezi sita endapo atakataa kuchanjwa pale inapotokea nchi inakabiliwa na mripuko wa magonjwa.
Suala la kuwalazimisha watu kuchanjwa kabla ya kutumia usafiri wa umma nchini humo limepingwa na waendeshaji huduma hizo.
Wenye vilabu vya pombe wameanza tena shughuli zao baada ya vizuizi vya kudhibiti kusambaa ugonjwa wa Corona kumalizika bila ya kutangazwa masharti mengine.
Waziri wa afya wa Uganda mnamo mwezi uliopita alisema zaidi ya chanjo 400,000 ziliharibiwa baada ya muda wao kumalizika bila ya kutumika.