1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa usalama wa viwanja vya ndege wagoma Ujerumani

Angela Mdungu
1 Februari 2024

Maafisa usalama wa viwanja 11 vya ndege nchini Ujerumani wamefanya mgomo wa siku moja, unaotarajiwa kusababisha kufutwa kwa zaidi ya safari 1,000 za ndege kote nchini humo. Mgomo huo utaathiri zaidi ya abiria 200,000.

Maandamano baada ya kuitishwa mgomo uwanja wa ndege wa Frankfurt
Hali katika uwanja wa ndege wa Frankfurt baada ya mgomo kuitishwa 01.02.2024Picha: Jörg Halisch/dpa/picture alliance

Mgomo huo ulianza Jumatano usiku katika uwanja wa ndege wa Cologne Bonn Magharibi mwa Ujerumani baada ya maafisa wa usalama wanaohusika na ukaguzi wa abiria kushindwa kutokea katika zamu zao za usiku.

Msemaji wa Chama Cha Umoja wa Wafanyakazi Ujerumani, Verdi, Bwana Özay Tarim amesema mgomo huo umeanza kwa mafanikio katika uwanja wa Cologne Bonn kwa wahusika kushiriki kwa asilimia 100%.

Chama cha wafanyakazi cha Verdi, kilitisha mgomo baada ya awamu kadhaa za mazungumzo kuhusu maslahi ya wafanyakazi na Chama Cha Makampuni ya Usalama wa anga BDLS kushindwa kupata makubaliano.

Madai hasa ni kuongezwa kwa mishahara kwa takribani €2.80 kwa saa. Kwa upande wake Chama Cha Makampuni ya Usalama wa Anga Ujerumani BDLS  kimesema kuwa walitoa pendekezo la kuongeza mshahara kwa asilimia 4% mwaka huu ikifuatiwa na ongezeko jingine la asilimia 3% mwaka ujao lakini chama cha wafanyakazi kililikataa.

Mgomo utasababisha kucheleweshwa kwa ndege zinazowasili

Viwanja vingine vya ndege vilivyokumbwa na mgomo huo wa maafisa wa usalama ni pamoja na Frankfurt, Hamburg, Bremen, Berlin, Leipzig, Düsseldorf, Cologne, Hanover, Stuttgart, Erfurt na Dresden baada ya maafisa wa chama cha wafanyakazi kuuitisha. Safari zote za ndege zinazoondoka zilifutwa katika viwanja vya ndege vya Berlin, Hamburg, Hanover na Stuttgart. Ndege zinazowasili, zinatarajiwa kuchelewa kwa kiasi kikubwa.

Maafisa wa kampuni binafsi za usalama wamegoma katika viwanja 11 vya ndege UjerumaniPicha: Jörg Halisch/dpa/picture alliance

Viwanja vya ndege vya kusini mwa jimbo la Bavaria kama vile  Munich na Nuremberg havijaathiriwa na mgomo huo kwani wafanyakazi wake wa usalama wanachukuliwa kuwa wafanyakazi wa sekta ya umma na wana mikataba tofauti. Uwanja mkubwa zaidi wa ndege wa  Ujerumani, Frankfurt, unatarajiwa pia kuwa na mvurugiko mkubwa wa shughuli zake Alhamisi ambapo tayari safari za abiria wanaliokuwa wakitarajia kuondoka zimefutwa mapema asubuhi.

Mgomo huu unafanyika ikiwa ni muda mfupi baada ya chama cha madereva wa treni wa Ujerumani  GDL kuitisha mgomo mrefu zaidi wa safari za treni wiki iliyopita.

Mgomo huo uliitishwa kufuatia mgogoro na kampuni ya uendeshaji wa huduma za reli Ujerumani Deutsche Bahn.

Chama cha wafanyakazi Verdi kimeitisha pia mgomo wa wafanyakazi wa huduma za usafiri wa umma karibu kote Ujerumani siku ya Ijumaa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW