1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiIran

Khamenei aongoza ibada za kuaga miili ya Raisi na maafisa

22 Mei 2024

Kiongozi wa juu nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei ameongoza ibada ya sala ya kuaga miili ya aliyekuwa Rais wa taifa hilo Ebrahim Raisi na maafisa wengine waliokufa kwenye ajali ya helikopta siku ya Jumapili.

Iran | Mazishi ya Ebrahim Raisi
Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa Iran wakiwa kwenye ibada ya swala ya kuwaaga Rais Ebrahim Raisi na maafisa wengine waliokufa kwenye ajali ya helikoptaPicha: Tasnim Agency

Khamenei ameongoza shughuli hiyo iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran. 

Vilio na maombolezo vikisikika kutoka kwa waombolezaji waliokusanyika kwa ajili ya kuwaaga viongozi wao. Majeneza yao yaliyokuwa yamezungushiwa bendera ya Iran, yalipangwa mbele ya maafisa wandamizi na mamia kwa maelfu ya waombolezaji.

Khamenei aliongozwa ibada ya  kawaida tu ya kuswalia maiti, akitumia lugha ya Kiarabu kama ilivyoandikwa kwenye kitabu kitakatifu cha Kiislamu cha Quran. Mara baada ya sala Khamenei aliondoka.

Rais wa mpito wa Iran Mohammad Mokhber aliyekuwa amesimama karibu na Khamenei alionekana akibubujikwa machozi wakati ibada hiyo ikiendelea.

Soma pia: Heshima za mwisho kwa Ebrahim Raisi zaanza kutolewa Iran

Baadaye, waombolezaji waliyabeba majeneza hayo mabegani huku wakipaza sauti "kifo kwa Marekani," kisha wakayaweka kwenye lori lililokuwa wazi tayari kuanza kutembezwa kwenye mitaa ya mji mkuu Tehran hadi Azadi ama Bustani ya Uhuru eneo ambako Raisi alikuwa akilitumia kuhutubia.

Maelfu ya waombolezaji mjini Tehran wakiwa wamejitokeza mjini Tehran kuaga miili ya aliyekuwa rais wao Ebrahim Raisi, waziri wa mambo ya nje na maafisa wengine wa Iran waliokufa kwenye ajali ya helikoptaPicha: Majid Asgaripour/WANA/REUTERS

Miongoni mwa waliohudhuria ni maafisa waandamizi wa Kikosi cha Walinzi wa Kimapinduzi, chenye ushawishi mkubwa nchini humo. Ismail Haniyeh, kiongozi wa wanamgambo wa Hamas wa Palestina pia alikuwepo. Ikumbukwe kundi hili linasaidiwa na Iran kijeshi katika vita vyake vinavyoendelea dhidi ya Israel katika Ukanda wa Gaza. 

Inasemekana maafisa wa ngazi za juu zaidi ya 40 kutoka mataifa ya kigeni watakuwepo mjini Tehran kwa ajili ya mazishi hayo.

Soma pia: Scholz atuma risala za rambirambi kwa Iran

Mwili wake hatimaye utasafirishwa hadi katika mji mtakatifu kwa waislamu wa madhehebu ya Shia wa Qom. Kutoka hapo, utarejeshwa kwenye mji mkuu Tehran na kuwekwa kwenye Msikiti Mkuu wa Mosalla kabla ya kupelekwa nyumbani kwake huko Mashahd, mashariki mwa Iran kwa mazishi kesho Alhamisi.

Kifo chake kinatokea wakati kukishuhudiwa mgawanyiko mkubwa kati ya uongozi wa kidini na kwa kiasi kikubwa jamii ya Iran, kuhusiana na udhibiti mkali wa masuala ya kijamii na kiuchumi na kusababisha hali kuwa ngumu.

Soma pia: Iran kufanya uchaguzi mkuu wa rais mnamo Juni 28

Rais Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amirabdollahian na maafisa wengine walikuwa wakirejea Iran, wakitoka kuzindua bwawa lililoko kwenye mpaka kati ya Iran na Arzebaijan siku ya Jumapili wakati helikopta yao ilipoanguka kwenye maeneo ya milima iliyopo mkoa wa Varzaghan.