1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa michezo nchini Nigeria walaumiwa kwa uzembe

14 Agosti 2024

Maafisa wa michezo nchini Nigeria wamelaumiwa kwa uzembe baada ya nchi hiyo kushindwa kupata medali yoyote katika mashindano ya Olimpiki.

Elizabeth Anyanacho
Elizabeth Anyanacho kutoka Nigeria aliyeshiriki michezo ya Taekwondo Picha: DW

Waziri wa Michezo wa Nigeria John Owan Enoh, ametoa wito wa kufanywa marekebisho baada ya Nigeria kuwa na matokeo mabaya kwenye mashindano ya Olimpiki mjini Paris.

Waziri huyo amesema wakati mataifa madogo barani Afrika yalirudi nyumbani na medali kadhaa, taifa lake kubwa liliambulia patupu kwa mara ya kwanza tangu kufanyika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2012 jijini London.

Mwanaridha wa Ethiopia ashinda medali ya dhabau katika mbio za Marathon

Licha ya kuwahusisha wanariadha wake ambao ni mabingwa barani Afrika kama vile Tobi Amusan anayeshikilia rekodi ya mbio za mita 100 kuruka viunzi, taifa hilo halikufikia matarajio ya Olimpiki.

Waziri wa Michezo John Owan Enoh amesema nchi yake inahitaji kutafuta mbinu mpya na pia kuhakikisha kwamba wanaoendesha michezo ni watu walio na uwezo mkubwa kiufundi, wazoefu na wazalendo, ili kubadili matokeo mabaya kama yaliyoshuhudiwa katika michezo ya Olimpiki ya mwaka Paris 2024.