1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Maafisa wa serikali Tanzania wapuuza uvaaji barakoa

George Njogopa25 Februari 2021

Licha ya serikali ya Tanzania kukiri kuwepo kwa janga la virusi vya corona nchini humo, viongozi wengi wakiwemo mawaziri wameendelea kupuuza umuhimu wa kuvaa barakoa. Wananchi wasema wanaonesha mfano mbaya.

Tansania Dar es Salaam | Kassim Majaliwa
Picha: Tanzania Presidents Office

Ni nadra sana kumkuta kiongozi wa kiserikali nchini Tanzania akiwa amevaa barakoa kama njia ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona, hata kama kiongozi huyo yupo kwenye majukumu yanayokusanya umati mkubwa wa watu.

Wakati wote viongozi hao wanaonekana kutokuwa na wasiwasi wakiendelea kutangamana na watu wa aina mbalimbali na hata wakati mwingine wakionekana kukaribiana mno.

Hali hiyo haiishii kwa vigogo hao, bali imeshuka mpaka nchini ambako wananchi wanaonekana kutolipa uzito suala la uvaaji wa barakoa na wanaendelea na shughuli zao kama ilivyo kawaida.

Rais Magufuli akizindua mradi wa kituo cha kimataifa cha mabasi jijini Dar es Salaam akiwa na maafisa waandamizi serikali bila hata mmoja wao kuvaa barakoa.Picha: Eric Boniphace/DW

Soma pia: Tanzania: Serikali zingatieni utaalamu kwenye chanjo

Hakuna ajuaye moja kwa moja hadi sasa kwa nini viongozi hao hawapendelei kutumia barakoa ingawa kumekuwa na udadisi wa hapa na pale ambao hata hivyo ni vigumu kuuthibitisha.

Kuwepo kwa minong'ono hiyo ya hapa na pale, kumemwibua pia naibu spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Akson Tulia ambaye wakati akishiriki ibada ya maziko, alikiri historia yake ya kuugua ugonjwa wa Covid-19 mara mbili.

"Mimi nimeishaumwa corona mara mbili, maana watu wanaweza kuhisi siijui, lakini kutokuvaa kwangu barakoa nachukuwa tahadhari nyingine," alisema Dk Tulia, ambapo alitoa hoja ya kwamba hata mazikoni hapo walikuwa wanatumia kipaza sauti kimoja watu tofauti.

Serikali haijakataza kuvaa barakoa

Hivi karibuni Rais John Magufuli alibainisha kuwa serikali yake haijapiga marufuku uvaaji wa barakoa lakini alitahadharisha juu ya kule zinakotoka.

Viongozi wakuu serikalini wakishiriki ibaada ya kumuaga aliekuwa katibu mkuu kiongozi John Kijazi pasina kuvaa barakoa.Picha: Said Khamis/DW

Wakati huu wa janga la corona ambalo limekuwa msiba wa dunia, viongozi wa serikali wamekuwa wakihimiza zaidi matumizi ya njia za asili kama vile mtindo wa kujivukiza pamoja na dawa za jadi kama baadhi ya njia za kukabiliana na tishio hilo.

Soma pia: COVID-19: Uingereza yapiga marufuku abiria kutoka Tanzania

Waziri wa afya, Donothy Gwajima anasema katika ziara yake ya kutembelea maeneo mbalimbali, kujionea namna ya uzalishaji wa dawa hizo, amejiridhisha pasina shaka kuwa kazi ya utumiaji wa nyezo hizo ni kubwa mnoo kwa wananchi.

"Na hatusemi kwamba wanapotumia bidhaa na huduma za tiba asili, eti wasiripoti kwenye vituo vya afya," alisema waziri Gwajima na kuongeza kuwa hizi ni huduma mbili zinazokwenda pamoja bila kuzuiwiliana.

Hadi sasa ingawa hakuna takwimu za moja kwa moja kutoka serikalini zinazoelezea vifo vitokanavyo ya janga hilo, lakini Tanzania imeendelea kurekodi kiwango cha kustaajabisha juu ya wale wanaopoteza maisha kutokana na kile kinachotajwa tatizo la upumiaji.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW