1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa waudhibiti moto Kanisa la Notre Dame mjini Paris

Sylvia Mwehozi
16 Aprili 2019

Rais Emmanuel Macron ameahidi kulijenga upya kanisa kuu katoliki la Notre Dame mjini Paris ambalo jana jioni lilishika moto ulio unguza sehemu ya jengo.

Frankreich, Paris: Brand in der Kathedrale Notre Dame
Picha: picture-alliance/AP/M. Euler

Rais Macron ameeleza kuwa sehemu kubwa ya jengo haikushika moto ambao wakati mmoja ulitishia kuteketeza jengo zima na kuiacha Ufaransa ikiwa katika mshutuko kutokana na uharibifu wa jengo linaloelezwa kuwa alama ya nchi hiyo. Moto uliozuka jana jioni umeharibu paa llililojengwa miaka 850 iliyopita ambalo ni thurathi ya dunia.

Mnara wa paa hilo uliteketea na kuanguka. Maafisa wapatao 400 wa zimamoto walihangaika usiku kucha kuuzima moto huo na hatimaye majira ya asubuhi walifanikiwa kuudhibiti na kulinusuru kanisa hilo zima lisiteketee. Mkuu wa kikosi cha zimamoto mjini Paris Jean-Claude Gallet alisema eneo muhimu la jengo hilo limeweza kuokolewa. Jengo hilo limekuwa na kazi za sanaa nyingi na ambazo kwa kiasi kikubwa zimeweza kuondolewa. Miongoni mwa hazina zilizomo ni taji la miiba ambalo hutolewa kwa nadra hadharani.

Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, lakini wakati ajali hiyo inatokea kanisa lilikuwa chini ya ukarabati ambao maafisa wa Zimamoto wanasema unaweza kuwa ndio chanzo. Rais Macron alikatisha hotuba yake juu ya sera na kwenda eneo la tukio.

Hali ilivyo baada ya moto kudhibitiwa katika kanisa la Notre DamePicha: Getty Images/AFP/S. de Sakutin

"Ninawaelezeni usiku huu; Tutajenga kanisa hili pamoja na bila shaka ni sehemu ya mustakabali wa Ufaransa na mradi wa baadae. Lakini nina dhamira hiyo. Kuanzia kesho, tutazindua kampeni ya kitaifa ya kuchangia na nje ya mipaka yetu tutawaendea watu walio na talanta kubwa zaidi na watu wengi watachangia. Na tutalijenga tena. Tutalijenga Notre Dame. Kwa sababu hayo ndio matarajio ya Wafaransa na kwa sababu historia yetu inastahiki hilo, kwa sababu ni hatma ya msingi wetu. Asante", alisema Macron.

Ujenzi wa kanisa la Notre Dame ulikamilika katikati mwa karne ya 12 baada ya miaka 200 ya kulifanyia kazi. Wakati wa mapinduzi ya Ufaransa karne ya 18, kanisa hilo lilivamiwa katika vurugu dhidi ya kanisa katoliki na kuharibiwa.  Ajali hiyo imetokea katikati mwa matayarisho ya wiki takatifu kuelekea sikukuu ya Pasaka. Waumini kadhaa walionekana wakipiga mgoti na kusali wakati juhudi za kuudhibiti moto zikiendelea.

Viongozi mbalimbali wa kidunia wametuma salamu za pole ikiwemo Vatican, ambayo imetoa taarifa ikieleza kushutushwa na masikitiko juu ya ajali hiyo ya moto. Jijini Washington rais Donald Trump kupitia ukurasa wake wa Twita, aliandika kuwa "inaumiza kuona moto mkubwa ukiteketeza kanisa la Notre Dame”, lakini kauli yake ya kutumuia matanki ya maji kukabiliana na moto huo ilizua sintofahamu.

Kansela Angela Merkel naye ametuma salamu za pole akilielezea kanisa kuwa alama ya Ufaransa na kitambulisho cha utamaduni wa ulaya nzima.

AFP/DPA/AP