Maafisa zaidi wa FIFA wakamatwa kwa madai ya rushwa
3 Desemba 2015Maafisa hao wawili kutoka bodi hiyo ya kandanda duniani walikamatwa leo (03.12.2015) katika msako uliofanywa mapema alfajiri katika hoteli ya kifahari ya Baur au Lac ilioko mjini Zurich, hii ni kulingana na maafisa wa serikali waliothibitisha kukamatwa kwao.
Hoteli ya Baur au Lac ndio hoteli waliokamatwa pia maafisa wengine kadhaa wakuu wa shirikisho hilo tarehe 27 mwezi Mei.
Hata hivyo Wizara ya sheria ya Uswisi haijawatambua watu hao wawili waliokamatwa lakini vyanzo kadhaa vya habari vimewatambua kama Naibu maraisi wa FIFA, Juan Angel Napout wa Paraguay na Alfredo Hawit Banegas wa Honduras.
Katika taarifa yake wizara hiyo imesema washukiwa hao wawili wanadaiwa kuchukua rushwa ya mamilioni ya dola, na kwamba fedha hizo zilihusishwa na haki za mauzo kwa michezo ya kuwania kombe la dunia na kombe la mataifa ya kusini mwa America - Copa America. Wawili hao bado wanazuiliwa na polisi wakingoja kusafirishwa Marekani.
Uvamizi wa siku ya Alhamisi umefanywa ikiwa ni mpango wa Marekani kufanya uchunguzi juu ya kashfa ya Ufisadi ndani ya shirikisho hilo la FIFA.
Maafisa wasemekana kuendesha shughuli za rushwa Marekani
Ombi la kukamatwa kwao lilitolewa na Marekani kwa sababu baadhi ya makosa yanayowakabili yalipangwa na kutekelezwa nchini humo. Wizara hiyo ya sheria nchini Uswisi imesema, malipo pia yalifanywa kupitia mabenki ya Marekani.
Uvamizi huo ulifanyika wakati wa mkutano wa siku mbili wa kamati kuu ya FIFA unaonuiwa kuweka mikakati ya mageuzi katika shirikisho hilo la kandanda ulimwenguni ambalo limezongwa na kashfa ya rushwa.
Kwa upande wake FIFA imesema kupitia taarifa yake kuwa inafahamu hatua iliyochukuliwa na idara ya haki ya Marekani na kwamba itashirikiana vilivyo na uchunguzi wa Marekani na Uswisi.
Sakata hilo la rushwa limesababisha kusimamishwa kazi kwa siku 90 rais wa muda mrefu wa FIFA Sepp Blatter, ambaye kwa sasa yuko chini ya uchunguzi nchini Uswisi kwa madai hayo hayo ya rushwa.
Michel Platini, mtu aliyedhaniwa kuwa mrithi wa Blatter katika nafasi hiyo ya raisi wa FIFA amesimamishwa kazi kwa muda na pia anachunguzwa kwa madai sawa na Blatter. Wote wawili huenda wakaondolewa kabisa katika shughuli za kandanda katika uamuzi unapotarajiwa kutolewa baadaye mwezi huu.
Mwandishi: Amina Abubakar
Mhariri: Yusuf Saumu