1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maalim Seif ajiunga na ACT Wazalendo

18 Machi 2019

Nchini Tanzania mwelekeo mpya wa kisiasa umejitokeza baada ya aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad kujiunga na chama kingine cha upinzani, ACT Wazalendo.

Seif Sharif Hamad
Picha: DW/S. Khamis

Chama cha ACT Wazalendo kinaongozwa na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe. Maalim Seif amechukua hatua hiyo muda mfupi baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliompa ushindi mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba. 

Mwanasiasa huyo mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za visiwani Zanzibar amehama na baadhi ya wanasiasa waandamizi waliokuwa wakimuunga mkono na amechukua uamuzi huo baada ya mvutano kati yake na mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba kutolewa uamuzi wa Mahakama Kuu na kumpa ushindi msomi huyo kuendelea na jukumu lake la uwenyekiti.

Ingawa awali kulikuwa na fununu juu ya uwezekano wa mwanasiasa huyo kujiunga na chama hicho, kutokana na mvutano mkubwa uliokuwa ukishuhudiwa ndani ya CUF, lakini hilo lilibidi kusubiri hadi pale alipolithibitisha mwenyewe wakati alipokutana na waandishi wa habari.

Kujiondoa kwa Maalim Seif katika chama alichodumu nacho kwa zaidi ya miongo minne kunatarajia kuandika historia mpya katika medani za siasa visiwani Zanzibar na huenda hili likathibitika zaidi katika uchaguzi mkuu ujao.

Maalim Seif ambaye kwenye chaguzi zilizopita amekuwa akilalamika kupokwa ushindi na mwanasiasa anayekubalika kwenye matabaka ya aina nyingi hajaeleza bayana kuhusu wabunge wanaomuunga mkono ambao bado wako ndani ya CUF. 

Hatua ya Maalim Seif kukihama chama chake ni mwendelezo wa matukio ya hivi karibuni yanayoendelea kuzipamba siasa za Tanzania, jambo ambalo halijawashangaza hata wachunguzi wa mambo.

Hivi karibuni aliyekuwa mgombea wa upinzani kwa umoja wa Ukawa, Edward Lowassa alirejea tena chama tawala CCM, katika kile alichodai kuwa aliamua kurejea nyumbani. 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW