1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi, malaria, na utapia mlo sababu za vifo DRC: WHO

28 Desemba 2024

Malaria na maambukizi ya kawaida ya mfumo wa upumuaji, yakichochewa na utapia mlo, yamesababisha wimbi lisilofahamika la vifo kusini-magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Shirika la Afya Duniani limesema.

DR Kongo | Afya
Congo imekuwa katika tahadhari ya afya kufuatia matukio yasiojulikana na ugonjwa.Picha: Al-hadji Kudra Maliro/AP Photo/picture alliance

DR Congo ilitangaza mapema mwezi huu kuwa ipo katika "hali ya tahadhari ya juu" kufuatia "tukio lisilojulikana la afya ya umma" lililosababisha vifo vya watu wengi katika eneo la Panzi, takriban kilomita 700 (maili 435) kusini-mashariki mwa mji mkuu, Kinshasa.

Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano walichangia takriban nusu ya visa na vifo vilivyotokana na kile kilichokuwa kikielezwa kama ugonjwa usiofahamika.
Hali hiyo ilianza kuonekana mwishoni mwa Oktoba, na mamlaka za afya za Panzi zilitangaza tahadhari mwishoni mwa Novemba kufuatia ongezeko la vifo.

Ufuatiliaji uliimarishwa haraka, ambapo, kwa kukosekana kwa utambuzi wa wazi, ulizingatia kufuatilia visa vya wagonjwa waliokuwa na homa, kikohozi, udhaifu wa mwili, na dalili kama baridi, maumivu ya kichwa, na ugumu wa kupumua, Shirika la Afya Duniani lilisema.

Katika taarifa ya hali hiyo, WHO ilisema kuwa kati ya Oktoba 24 na Desemba 16, jumla ya visa 891 vilikidhi ufafanuzi huo, na vifo 48 viliripotiwa.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilisema kuwa kufikia Desemba 16, matokeo ya maabara kutoka kwa sampuli 430 yalionyesha matokeo chanya kwa malaria na virusi vya kawaida vya mfumo wa upumuaji, ikijumuisha mafua, rhinovirusi, SARS-CoV-2, virusi vya korona vya binadamu, virusi vya parainfluenza, na adenovirusi ya binadamu.

Hospitali Kuu ya Panzi ambako vifo vingi vimnetokea.Picha: Lucien Lufutu/AP/picture alliance

Soma pia: Ugonjwa usiojulikana nchini Kongo umesababisha vifo vya watu kadhaa.

"Ingawa vipimo vya maabara vinaendelea, matokeo haya kwa pamoja yanapendekeza kuwa mchanganyiko wa maambukizi ya kawaida na ya msimu ya mfumo wa upumuaji na malaria ya falciparum, yakichochewa na utapia mlo mkali, ulisababisha ongezeko la maambukizi makali na vifo, hasa miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano," WHO ilisema.

"Tukio hili linaangazia mzigo mkubwa unaotokana na magonjwa ya kawaida ya kuambukiza (maambukizi makali ya mfumo wa upumuaji na malaria) katika muktadha wa jamii zilizo hatarini zinazokabiliwa na uhaba wa chakula," iliongeza.

WHO ilitathmini kuwa hatari ya jumla kwa afya ya umma katika jamii zilizoathiriwa ni kubwa, ikihitaji udhibiti madhubuti wa malaria na kuboresha lishe.
Kwa kiwango cha kitaifa, hatari ilizingatiwa kuwa ndogo kutokana na hali ya tukio hilo kuwa la eneo fulani pekee.

Kongo yaanza kampeni ya chanjo ya Ebola

00:45

This browser does not support the video element.

"Hata hivyo, maeneo mengine mengi ya DRC yanakabiliwa na viwango vya juu vya utapia mlo, na kile kilichoshuhudiwa Panzi kinaweza pia kutokea mahali pengine nchini," WHO iliongeza.

Soma pia: Ugonjwa usiofahamika wauwa watu 143 DRC

Upatikanaji wa eneo hilo ni mgumu kwa barabara, na miundombinu ya afya ni duni. Wakazi pia wanakabiliwa na uhaba wa maji ya kunywa na dawa.

Kulingana na mamlaka za Congo, eneo hilo, ambalo lilipata mlipuko mbaya wa homa ya typhoid miaka miwili iliyopita, lina moja ya viwango vya juu vya utapia mlo nchini, kwa asilimia 61.
DRC, moja ya nchi maskini zaidi duniani, imekuwa katika miezi ya hivi karibuni kitovu cha mlipuko wa mpox, na zaidi ya vifo 1,000 kuripotiwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW