1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya corona yamepindukia milioni 100 ulimwenguni

27 Januari 2021

Maambukizi ya virusi vya corona vimepindukia milioni 100 ulimwenguni huku leo hii ikifikia mwaka mmoja tangu kisa cha kwanza kuripotiwa Ujerumani.

Coronavirus | Impfstoff und Impfzentren
Picha: Martin Wagner/imago images

Kisa cha kwanza Ujerumani Kiliripotiwa tarehe 27.01 mwaka 2020 ambapo mfanyikazi wa kampuni ya iliyoko Munich alipatikana na Corona, na kifo cha kwanza cha COVID-19 kiliripotiwa mnamo Machi 8. Siku mbili baadaye, kulikuwa na maambukizo katika majimbo yote 16. Tangu wakati huo, hakuna chochote kilichobaki sawa.

Katika siku chache, hatua kali ziliwekwa Ujerumani, migahawa na sinema zilifungwa, pamoja na shule na chekechea. Shughuli za kibiashara nazo pia zilisitishwa kwa muda.

Bunge la Ujerumani pia lilipitisha euro bilioni 156 kukabiliana na janga hilo na kutokana na kufungwa kwa usafiri , watu wengi walipata nafasi yao ya kwanza ya kufanyia kazi nyumbani.

Maduka makubwa yalibaki wazi lakini walioruhusiwa kuingia walilazimika kuvaa barakaoa, hofu ya kununua bidhaa mbali mbalimbali ilianza huku baadhi zikiwa chache.

Mnamo Machi 18, Kansela Angela Merkel alihutubia taifa kupitia runinga. "Ni jambo zito. lichukueni kwa uzito. Sio tangu kuungana tena kwa Wajerumani, hapana, tangu Vita vya Kidunia vya pili ambapo nchi hii inakabiliwa na changamoto ambayo inatuhitaji kuchukua hatua za umoja kwa pamoja." alisema Merkel.

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Hannibal Hanschke/REUTERS

Idadi inaendelea kuongezeka

Kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita Marekani imerekodi zaidi ya visa milioni 25 na taifa hilo linasalia kuwa lenye mambukizo makubwa zaidi na idadi kubwa zaidi ya vifo.

Idadi ya visa vilivyorekodiwa na takwimu zilizotolewa na wakala wa kitaifa wa Afya, inawakilisha sehemu ndogo tu ya maambukizi halisi kwani virusi vya corona vimeenea ulimwenguni kote.

Rais Mpya wa Marekani Joe Biden hata hivyo ameahidi kuzidisha mikakati ya mpango wa utengenezwaji na usambazaji wa chanjo.

Biden anajaribu kugeuza mapambano dhidi ya virusi vya corona, ambavyo wakati wa utawala wa rais Donald Trump kulikuwa na taarifa mseto kuhusu uvaaji wa barakoa pamoja na tahadhari za kusambaa kwa virusi hivyo. 

Rais wa Marekani Joe Biden na Tabe Masa, Muuguzi na Mkuu wa Huduma za Afya ya wafanyikaziPicha: Alex Edelman/AFP

Vigezo vikali zaidi

Biden amesema kutoa chanjo kwa watu wote wa Marekani ni changamoto kubwa, na mpango uliorithiwa kutoka kwa utawala wa Trump "ulikuwa katika hali mbaya kuliko walivyotarajia.

Uingereza nayo pia idadi ya visa vya COVID-19 imepindukia 100,000, huku mataifa mengine ya Ulaya yakizingatia kuimarisha mipaka yao kwa matumaini ya kufungia nje virusi vipya vinavyosambaa kwa kasi zaidi.

Kulingana na gazeti la London Times, serikali ya Uingereza itatangaza kwamba wasafiri wa lazima wakae karantini katika hoteli karibu na viwanja vya ndege kwa siku 10 baada ya kurudi kutoka nchi 30 zilizo hatarini, haswa Amerika Kusini na Kusini mwa Afrika.

Ireland kwa mara ya kwanza imeanzisha sheria ya karantini za lazima kwa wanaoingia nchini humo, na pia kuongeza hatua za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona hadi Machi 5.

Miongoni mwa mataifa mengine ya Ulaya yanayopanga kuimarisha udhibiti wa mipaka ni Ujerumani, ambayo kwa sasa inazingatia kusitisha kabisa safari za ndege kuingia nchini. Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer amesema hatari za aina mpya virusi vya corona inawalazimisha kuzingatia kuweka vigezo vikali zaidi.

Kampeni ya usambazaji chanjo inayumba

Picha: Maja Hitij/Getty Images

Kampeni ya chanjo ya Ulaya inalegelega baada ya kampuni ya AstraZeneca kuonya kuwa haitaweza kufikia malengo yaliyoahidiwa juu ya usafirishaji wa chanjo hiyo kwa matifa ya Umoja Ulaya wiki moja tu baada ya kampuni ya Pfizer kusema pia inachelewesha kiwango cha usambazi wa chanjo ya COVID-19.

Kutokana na pengo lililopo katika usambazaji wa chanjo kati ya mataifa tajiri na masikini umekosolewa vikali na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ambao wametoa mwito wa uwepo wa usawa katika upatikanaji wa chanjo ya COVID-19.

Viongozi wa jamii ya Kiyahudi wanasema kwamba janga hilo limezidisha chuki Ujerumani, huku Uturuki na Sweden zikiongeza muda wa vizuizi ili kudhibiti maambukizi.

 

AFP/dpa/Reuters/  https://p.dw.com/p/3oRJu