1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Watu 80,430 waambukizwa corona katika saa 24

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
12 Januari 2022

Maambukizi ya virusi vya corona ya kila siku yamefikia viwango vya juu hapa nchini Ujerumani ambako kufikia sasa zaidi ya watu elfu 80,000 wameambukizwa katika siku moja tangu lilipoanza janga la corona.

Berlin, Deutschland | Impfstation
Picha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

Mamlaka za afya nchini Ujerumani zimeorodhesha idadi ya watu 80,430 walioambukizwa virusi vya corona katika muda wa saa 24 zilizopita. Kulingana na takwimu kutoka kwenye Taasisi ya kupambana na magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch, maambukizi ya hivi punde yaliongezeka kwa zaidi ya watu 21,500 kulinganisha na wiki iliyopita.

Wakati huo huo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz atajibu maswali ya wabunge leo hii ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu achukue hatamu za ukansela atajibu masswali ya wabunge kwenye mjadala unaotazamiwa kuwa mkali kuhusu jinsi na lini serikali yake ya mesto inakusudia kutangaza agizo la kitaifa juu ya ulazima wa kila mtu kupata chanjo dhidi ya COVID-19. 

Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Hannibal Hanschke/REUTERS

Mjadala huo umepamba moto katika siku za hivi karibuni, na upande wa upinzani unaituhumu serikali kwa kuchelewa kueleza mpango wa wazi juu ya swala hilo lenye utata. Mahojiano ya kwanza ya kansela Olaf Scholz bungeni, yanatarajiwa kudumu kwa dakika 65 ambapo pia maswala ya sera ya ndani, kimataifa na hali ya hewa yatashughulikiwa miongoni mwa masuala mengine.

Kwa upande wake Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ametoa mwito wa kuchunguzwa kwa kina mjadala juu ya mipango ya chanjo ya lazima nchini Ujerumani akisema hatua hiyo inahitaji kujadiliwa kwa upana kabla ya kuthibitishwa.

Kwingineko duniani Marekani inakabiliwa na kuongezeka kwa idadi ya watu walioambukizwa na wale waliolazwa hospitalini kwa ajili ya kuugua COVID-19. Dk. Anthony Fauci Mshauri Mkuu wa Matibabu wa Rais wa Marekani amesema Marekani inaorodhesha karibu watu milioni moja wanaopata COVID-19 kwa siku, na zaidi ya watu 1,200 wanakufa kwa ugonjwa huo kila siku. Amesema watu wapatao laki moja na elfu 50 wamelazwa hospitalini lakini ana matumaini kwamba Marekani itafikia hatua mpya ambapo kutakuwa na ulinzi wa kutosha kwa jamii na dawa za kutosha zitapatikana.

Dk. Anthony Fauci Mshauri Mkuu wa Matibabu wa Rais wa MarekaniPicha: Michael Brochstein/ZUMA Press Wire/Zumapress/picture alliance

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limesema kutolewa nyongeza za chanjo kwa kutumia chanjo za asili za COVID-19 haukuwa mkakati mzuri wa kupambana na kirusi kipya cha omicron. WHO imetoa mwito wa kutumiwa chanjo mpya zitakazotoa ulinzi bora dhidi ya maambukizi ya corona. Mkakati wa chanjo kulingana na nyongeza za mara kwa mara kwa kutumia muundo wa awali wa chanjo hauwezi kuwa sahihi au endelevu wamesema washauri cha chanjo cha WHO.

Huko Korea Kusini wizara ya afya kuanzia leo Jumatano imezindua matumizi ya chanjo ya Novavax dhidi ya COVID-19 na nchi hiyo pia inajiandaa kusambaza dawa ya kumeza ya Pfizer inaoitwa Paxlovid ikiwa ni mbinu za ziada za kulikabili tishio la kirusi cha omicron.

Na takriban Wanyarwanda mia moja wameripotiwa kuvuka na kuingia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika siku za hivi karibuni, wakisema wanaikimbia nchi yao kwa sababu ya sheria za chanjo ya Covid-19.

 Afisa mmoja katika kisiwa cha kusini cha Idwi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kundi dogo la raia wa Rwanda, waliosafiri kwa kutumia mtumbwi, wako kwenye ukingo wa kisiwa hicho kilichopo kwenye Ziwa Kivu lililo kwenye mpaka wa Karongo Kalaja.

Vyanzo:AP/DPA/AFP/Permalink https://p.dw.com/p/45PLV