1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya virusi vya corona yafikia milioni moja

Sekione Kitojo
3 Aprili 2020

Vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19, vinaongezeka kwa kasi ya kutisha nchini Uhispania, Italia na mjini New York, eneo ambalo limeathirika zaidi nchini Marekani.

Coronavirus USA New York Ambulanzfahrzeuge NYU Langone Hospital
magari ya kubebea wagonjwa nje ya kituo cha matibabu ya dharura katika hospitali ya Langone mjini New York Picha: Reuters/B. McDermid

Kufikia leo Ijumaa ugonjwa  huo umewakumba zaidi ya watu milioni  moja duniani kote. Na watu  milioni 10 wamepoteza  ajira nchini Marekani kutokana na  ugonjwa wa COVID-19.

Maiti zikitolewa kutoka katika gari kwa kutumia mashine ya kubebea mizigo katika hospitali ya Brooklyn mjini New YorkPicha: picture-alliance/dpa/AP/J. Minchillo

Mzozo wa  kiafya  unaongezeka  mjini  New York , ambako  kampuni moja  ya  mazishi  katika  eneo  ambalo  limeathirika  zaidi , lilikuwa na  miili  185 iliyolundikana , zaidi  ya  mara tatu  ya uwezo wake wa kawaida. Mji  huo umeshuhudia  takriban vifo 1,500 kutokana  na virusi hivyo.

Duniani  kote  idadi ya  maambukizi  yaliyoripotiwa  imefikia katika hali ya  kutisha ya watu milioni moja, ambapo watu 53,000 wamefariki, kwa  mujibu  wa  data kutoka chuo kikuu  cha  Johns Hopkins.

Lakini  idadi  halisi  inaaminika  kuwa  juu  zaidi  kwasababu  ya ukosefu  wa  vifaa  vya uchunguzi, wakati  kesi ndogo  ndogo  nyingi haziripotiwi, na  nchi  kadhaa  zinaficha kiwango  cha  maambukizi.

Mazishi nchini Uhispania katika makaburi ya santa Margarida de Montbui. Wafanyakazi wakizika wahanga wa virusi vya corona huku jamaa za wahanga hao wawili tu wakiruhusiwa kushuhudia.Picha: Imago-Images/Agencia EFE/S. Saez

Uhispania  jana  iliripoti  idadi ya  juu  kabisa ya  vifo  kwa  siku, ambapo watu 950 walifariki, na  kufikisha  idadi ya  jumla  ya  watu waliofariki kufikia 10,000, licha  ya  ishara  kuwa  kiwango cha maambukizi  kinapungua. Italia  imerekodi vifo 760, na  kufikisha idadi  ya  vifo 13,900, ikiwa  ni  hali  mbaya  kabisa  kuliko  nchi yoyote, lakini  maambukizi  mapya  yanaendelea  kupungua  pia.

Idadi ya vifo yaongezeka

Ufaransa  imerekodi  jumla  ya  vifo  4,500  katika  hospitali, ambapo  vifo 471  ni  katika  siku moja  iliyopita. Lakini  maafisa wanatarajia  idadi  jumla  ya  vifo  kuchupa  kwa  kiasi  kikubwa kwasababu  ndio  kwanza  wanaanza  kuhesabu  vifo  katika majumba  ya  kuwahifadhi  wazee pamoja  na  maeneo  mengine kwa  ajili  ya  wazee.

Baraza kuu  la  Umoja  wa Mataifa  jana  liliidhinisha  azimio  linalotoa wito  wa  ushirikiano  wa  kimataifa pamoja  na juhudi  za  pamoja katika  kupambana na  ugonjwa  wa  COVID-19, katika  waraka  wa kwanza  kutolewa  na  chombo hicho  cha  kimataifa tangu kuzuka kwa  ugionwa  huo.

Azimio hilo lililoidhinishwa  kwa  kauli moja , pia  linasisitiza, "haja ya kuheshimu  haki za  binadamu" na  kwamba  "kuna nafasi  kwa  aina yoyote ya  ubaguzi, na chuki dhidi  ya  wageni  katika  kupambana na janga  hili."

Mfanyakazi akipulizia dawa ya kuuwa vijidudu katika eneo la wazi mjini Milan nchini Italia.Picha: AP

Urusi  ilishindwa  katika  juhudi  zake  za  kupinga azimio  hilo  kwa kutoa mswada wake  binafsi kwa  maelezo  kwamba umeungwa mkono  na  mataifa  manne.

Mashirika  ya  ndege  ulimwenguni yamepoteza  kiasi  ya  asilimia 80  uwezo wa  kubeba  abiria  kimataifa  ikilinganishwa  na  mwaka mmoja  uliopita na  nusu  ya  ndege  duniani  zimeegeshwa, data mpya  zinaonesha, zikieleza  kuwa  sekta  hiyo  ya  safari za  anga huenda  ikachukua  miaka  kurejea  katika  hali  ya  kawaida kutokana  na  janga  la  virusi  vya  corona.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW