1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Maambukizo ya UVIKO-19 yarudi upya China

28 Desemba 2022

Hospitali na nyumba za kutayarisha maziko nchini China zinaripotiwa kujaa wakati wimbi kubwa la maambukizo ya UVIKO-19 likizizidi nguvu huduma hizo katika taifa hilo la pili kwa nguvu za kiuchumi duniani.

China Corona-Pandemie | Huaian
Picha: cnsphoto via REUTERS

Licha ya kuripoti vifo vitatu tu vinavyotokana na UVIKO-19 siku ya Jumanne (Disemba 28), idadi hiyo inatajwa kutofanana na ile inayoripotiwa kutoka nyumba za kutayarishia maziko na pia uzoefu kutoka mataifa yenye idadi ndogo zaidi ya watu baada ya kufunguwa tena shughuli zao za kawaida.

Wafanyakazi katika hospitali ya Huaxi, ambayo ndiyo kubwa kabisa kusini magharibi mwa China, wanasema wamelemewa na wagonjwa wanaouguwa ugonjwa UVIKO-19.

Dereva mmoja wa gari la kubebea wagonjwa aliliambia shirika la habari la Reuters bila kutaja jina kwamba kwa miaka 30 ambayo amekuwa akifanya kazi hapo, hakuwahi kushuhudia kiwango cha sasa cha kulemewa.

Hadi jioni ya Jumanne, waandishi wa habari waliripoti kushuhudia misururu mirefu ya wagonjwa kwenye kitengo cha huduma za dharura na kliniki ya homa ya hospitali hiyo, huku wengi miongoni mwa wale waliofikishwa hapo na magari ya wagonjwa wakiwa wanasaidiwa kupumua kwa mashine.

Dawa zimekwisha

Mfanyakazi mmoja wa idara ya madawa aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba takribani wagonjwa wote hospitalini hapo walikuwa wa maambukizo ya korona.

Wasafiri wakiwa na barakowa katika Uwanja wa Ndege wa Beijing.Picha: Kyodo/picture alliance

"Hospitali ilikuwa imeishiwa na madawa maalum ya kutibuUVIKO-19 na badala yake inatowa tu vidonge vya kutibu ishara za ugonjwa huo kama vile kikohozi." Alisema.

Kwa upande mwengine, eneo la kuegesha magari kwenye nyumba ya kutayarisha maziko ya Dongjiao, ambayo ni miongoni mwa kubwa kabisa kusini magharibi mwa China, limejaa magari.

Maziko mfululizo

Shughuli za maziko zinafanyika mfululizo huku moshi kutoka eneo la kuchomea maiti ukijaa angani.

"Tunapaswa kufanya hivi mara 200 kwa siku sasa. Tumeelemewa mno kiasi cha kwamba hata muda wa kula hatuna. Hali imekuwa hivi tangu kufunguliwa. Kabla ya hapo ilikuwa ni wastani wa maiti 30 mpaka 50 kwa siku." Mmoja wa wafanyakazi wa hapo aliliambia shirika la habari la AFP.

Upimaji virusi vya korona ukiendelea jijini Beijing.Picha: Noel Celis/AFP/Getty Images

Hali kama hiyo imeripotiwa pia kwenye hospitali na nyumba nyengine za kutayarisha maziko maeneo mbalimbali nchini China, huku serikali ikisema kuwa inahisabu kifo kuwa kimetokana na UVIKO-19 pale tu mgonjwa anapokuwa amefariki kutokana na homa ya mapafu ama kushindwa kupumua.

Zhang Yuhua, afisa katika Hospitali ya Chaoyang jijini Beijing, alisema wagonjwa wengi ni ama wazee sana au wanauguwa maradhi mengine yaliyo thakili, ambapo "idadi yao imeongezeka kufikia wastani wa 450 hadi 550 kwa siku, kutoka 100 walivyokuwa kabla."
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW