1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandalizi ya COP28 yaanza Bonn

5 Juni 2023

Mazungumzo ya siku 10 yanaanza mjini Bonn ikiwa sehemu ya maandalizi ya ngazi za juu ya mkutano wa kimataifa wa mazingira, COP28, ambao utafayika katika Umoja wa Falme za Kiarabu miezi sita ijayo.

Petersberg Climate Dialogue | Berlin | 2023
Picha: JOHN MACDOUGALL/AP/picture alliance

Wawakilishi kutoka mataifa na mashirika zaidi ya 50 wanakutana hapa mjini Bonn kupanga Mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba jijini Dubai. 

Mkuu wa kitengo cha Mabadiliko ya Tabianchi cha Umoja wa Mataifa, Simon Stielli, aliliambia shirika la habari la dpa kwamba ni jukumu la mkutano huo kuhakikisha "dunia inafanikiwa kuzuwia kiwango cha joto la ulimwengu kwenye nyuzi 1.5 kwa kipimo cha Celsius, na kwamba mkutano utakaofanyika Dubai utakuwa na nafasi ya kufanya mageuzi makubwa yanayohitajika.

Soma zaidi: UAE yamteua bosi wa shirika la mafuta kuongoza COP28

Washiriki wa mikutano inayoanza leo (Jui 5) mjini Bonn wanatazamia mkuu wa Shirika la Mafuta la Abu Dhabi, Sultan al-Jaber, ambaye amechaguliwa kuwa rais wa wa COP28, atawasilisha mpango madhubuti wa jinsi urais wake utakavyokuwa na manufaa kwenye mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Nje ya ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Kimataifa cha Bonn, wanaharakati na wanasheria wanatazamiwa kupaza sauti zao kupinga uteuzi wa Jaber, wakimtaka ajiuzulu wadhifa huo. 

Wiki chache zilizopita, zaidi ya wabunge 100 wa Bunge la Marekani na Bunge la Ulaya waliotoa tamko la pamoja kutaka Jaber aondoshwe kwenye urais wa mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP28.

Upinzani dhidi ya Jaber

Mkuu wa Mfuko wa Tabianchi wa Ulaya, Laurence Tubiana, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba Jaber anapaswa kuonesha yalipo matakwa yake waziwazi na kwa haraka, kwani japokuwa nishati jadidifu ni muhimu lakini kutambua pekee hakutoshi bila kuchukuwa hatua madhubuti sasa. 

Viongozi wa baadhi ya mataifa ya dunia wakiwa na Rais wa Mkutano wa COP28, Sultan Al Jaber (katikati) mjini Berlin.Picha: JOHN MACDOUGALL/AFP/Getty Images

Mkuu huyo wa shirika la mafuta la Abu Dhabi anapendelea maendeleo ya haraka ya nishati jadidifu ingawa analaumiwa kwa kupendekeza kukabiliana na upunguzaji wa gesi chafu kwa kutumia teknolojia zenye utata badala ya kupunguza matumizi ya nishati za visukuku, akisisitiza kuwa nishati hizo zina jukumu kubwa kwenye kipindi cha mpito.

Soma zaidi: Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani atahadharisha juu ya kusawazisha uhusiano na rais wa Syria bila ya kumpa masharti.

Hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Sheikh Abdullah bin Zayed Al-Nahyan, ambaye ana dhamana ya kusimamia matayarisho ya COP28, alikutana na mjumbe maalum wa rais wa Marekani kwenye masuala ya tabianchi, John Kerry, katika mkutano uliohudhuriwa pia na Jaber. 

Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo ilisema kwamba ulipitia miradi ya pamoja kati ya nchi hizo mbili, ukiwemo ushirikiano wa kuharakisha kipindi cha mpito kuelekea nishati salama, kwa kifupi, PACE, ambao unagharimu dola bilioni 100 za Kimarekani.

Vyanzo: dpa, AFP
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW