1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandalizi ya Kombe la Mataifa Afrika yaendelea

29 Desemba 2014

Maandalizi ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika yanaendelea, wakati timu inayopigiwa upatu kutoroka na kombe hilo Algeria imetaja kikosi chake cha mwisho kwa ajili ya fainali hizo mwakani nchini Guinea ya Ikweta

WM Qualifikation Algerien Training
Picha: F.Batiche/AFP/GettyImages

Mahasimu wao katika kundi C Ghana na Afrika kusini hazijaamua nani atakuwamo katika vikosi vyao. Kocha mpya wa Ghana Avram Grant, ambaye aliiongoza Chelsea katika fainali ya kombe la Champions League mwaka 2008 na kushindwa kwa penalti dhidi ya Manchester United , amechagua kikosi cha kwanza cha wachezaji 31.

Kocha wa Afrika kusini , Ephraim "Shakes" Mashaba , amewaita wachezaji 34 kwa ajili ya kambi ya mazowezi baada ya krismasi mjini Johannesburg.

Cape Verde , Gabon na Mali tayari zimekwisha chagua vikosi vyao vya mwisho kwa mashindano hayo ya kila baada ya miaka miwili yanayojumuisha timu 16 zinazopambana katika fainali hizo katika viwanja vya mjini Bata, Ebebiyin, Malabo na Mongomo nchini Guniea ya Ikweta.

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, mwenyeji Guinea ya Ikweta, Guinea na Cote D'Ivoire bado hazijataja vikosi vyao kabla ya muda wa mwisho wa Januari 7 wa kutangaza vikosi vyote vitakavyoshiriki katika fainali.

Kocha wa Algeria mzaliwa wa Ufaransa Christian Gourcuff amewajumisha wachezaji 18 kati ya kikosi cha wachezaji 23 waliokwenda Brazil mwaka 2014 katika kombe la dunia na kuifikisha timu hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika duru ya mtoano kwa mara ya kwanza.

Grant amewaondoa kundini Kevin-Prince Boateng na Sulley Muntari, ambao waliondolewa katika kikosi cha kombe la dunia nchini Brazil, baada ya kudokeza kuwa angependa kuwaita tena wachezaji hao.

Mchezaji wa siku nyingi wa kati Michael Essien , ambaye alicheza chini ya Grant akiwa Chelsea , ni mchezaji nyota mwingine ambaye ameshindwa kuingia katika kikosi hicho.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae
Mhariri: Idd Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW