Taharuki yatanda Cameroon kabla ya matokeo kutangazwa
27 Oktoba 2025
Mamlaka zinasema maandamano yalizuka Jumapili baada ya mgombea wa upinzani Issa Tchiroma Bakary, aliyejitangazia ushindi wa asilimia 54.8 ya kura, kuwataka wafuasi wake waandamane kwa amani licha ya marufuku ya mikusanyiko ya umma.
Hata hivyo, wachambuzi wengi wanatarajia Rais Paul Biya mwenye umri wa miaka 92 kuibuka tena mshindi, hatua itakayorefusha zaidi utawala wake wa zaidi ya miaka arobaini madarakani.
Katika jiji kubwa zaidi la Douala, gavana wa mkoa wa Littoral, Samuel Dieudonné Ivaha Diboua, alithibitisha kuwa waandamanaji walivamia kituo cha walinzi wa usalama na vituo vya polisi, hali iliyosababisha vikosi vya usalama kuchukua hatua. "Kwa bahati mbaya watu wanne wamepoteza maisha,” akiongeza kuwa maafisa kadhaa wa usalama pia wamejeruhiwa.
Video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha polisi wakirusha mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wameziba barabara na kuchoma moto matairi. Mashuhuda waliiambia AFP kwamba risasi zilianza baada ya mabomu ya machozi, na miili mitatu ikaanguka karibu na kituo cha walinzi wa usalama.
Upinzani wasema serikali inatumia vitisho kwa wananchi
Upinzani na makundi ya kijamii yameishutumu serikali kwa kutumia vitisho na kukamatwa kwa watu ili kukandamiza sauti za wananchi. Watu wapatao 105 wanashikiliwa na polisi, huku viongozi wa upinzani wakidai kuwa makumi ya wafuasi na wanaharakati wamekamatwa katika siku za hivi karibuni.
Wakati matokeo yakisubiriwa, raia wanatumia mitandao ya kijamii kueleza wasiwasi wao katikati ya maandamanona ongezeko la mvutano juu ya madai ya wizi wa kura. Mwanaharakati wa mtandaoni Branson Maimo, akizungumza kutoka Douala, alielezea mitandao ya kijamii kama jukwaa muhimu la kujieleza katika taifa ambako kutoa maoni ya upinzani hadharani kunaweza kuleta hatari.
"Sasa hivi mitandao ya kijamii imekuwa maarufu zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Naona inazidi kukua mwaka hadi mwaka. Kwa hiyo tunaanza kupata sauti yetu, tunajipata na ujasiri wa kuelewa kwamba ni jukumu letu kufanya jambo kuhusu hali hii, kwa sababu hii ni nchi yetu na siasa zinamgusa kila mtu — iwe wewe ni daktari, fundi mabomba, mwendesha bodaboda, mjasiriamali kama mimi, mkulima, au kazi yoyote ile — maisha yetu kimsingi yanaamuliwa na siasa. Hivyo basi, tusipowawajibisha viongozi wetu, ni sawa na kuacha wengine watupangie maisha yetu ya baadaye, na hilo ni jambo hatari sana."
Serikali yasema maandamano ni sehemu ya uasi
Matokeo kutangazwa huku kukiwa na Katika miji ya Garoua na Maroua, maandamano yaligeuka kuwa ya vurugu wakati wafuasi wa Tchiroma walipokabiliana na polisi wakipiga kelele "Kwaheri Paul Biya, Tchiroma anakuja.” Kundi la ufuatiliaji wa mtandao NetBlocks liliripoti usumbufu mkubwa wa mtandao wa intaneti, hali inayoweza kuwa imepunguza upatikanaji wa taarifa kutoka eneo la tukio.
Waziri wa Utawala wa Ndani wa Cameroon, Paul Atanga Nji, alielezea maandamano hayo kuwa ni sehemu ya "mpango wa uasi” unaolenga kuidhoofisha nchi, akionya kuwa serikali haitavumilia vitendo vya vurugu.
Wachambuzi wanasema mvutano nchini Cameroon umeongezeka kwa wiki kadhaa, ukichochewa na hasira ya vijana na upinzani unaodai serikali imetumia nguvu za dola kupendelea upande wa Biya katika uchaguzi.
Uamuzi wa Biya kugombea tena akiwa na umri wa miaka 92, baada ya zaidi ya miongo minne madarakani, umeibua hasira zaidi miongoni mwa wananchi.
Baraza la Katiba linatarajiwa kutangaza matokeo rasmi ya uchaguzi huko Yaoundé. Hata hivyo, taifa liko katika hali ya taharuki, huku hofu ikitanda kwamba tangazo lolote litakalompendelea Biya linaweza kusababisha mlipuko mpya wa machafuko kote nchini.