1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano dhidi ya sheria mpya ya uraia India

Oumilkheir Hamidou
16 Desemba 2019

Maelfu ya watu wameteremka majiani katika miji kadhaa ya India , masaa machache tu baada ya dazeni kadhaa za waandamanaji na maafisa wa polisi kujeruhiwa, machafuko yaliporipuka katika viwanja vinavyozunguka vyuo vikuu.

Indien, Neu-Delhi: Protestierende Jamia Milia Islamia Studenten
Picha: DW/A. Ansari

Sheria ya uraia iliyoidhinishwa wiki iliyopita inawaruhusu wahamiaji ambao si waislam kutoka nchi tatu zenye wakaazi wengi wa kiislam, Afghanistan, Bangladesh na Pakistan kupata uraia ikiwa wanasumbuliwa kutokana na imani zao za kidini.

Wakosoaji wanasema sheria hiyo iliyowasilishwa na chama cha waziri mkuu Narendra Modi cha wazalendo wa kihindu -Bharatiya Janata ni dhidi ya waislam.

Watu wanne wameuwawa katika jimbo la kaskazini la Assam tangu maandamano yalipoanza wiki iliyopita.

Machafuko yameripuka jumapili baada ya maandamano ya wanafunzi kutoka chuo kikuu cha Jamia Milia Islamia mjini New-Delhi kugeuka mapambano dhidi ya vikosi vya polisi.

Polisi wametumia gesi za kutoa machozi na kuwakamata wanafunzi 100 kabla ya kuwaachia huru mapema jumatatu.

Watu wasiopungua 69 wakiwemo waandamanaji 39 na polisi 30 wamejeruhiwa na mabasi yasiyopungua manne na pikipiki 100 zimetiwa moto-msemaji wa polisi MS Radahawa amesema .

Waandamanaji wanadaai mitandao ifunguliwePicha: Surender Kumar

 Korti kuu inatarajiwa kuamua jumanne kama sheria hiyo ni halali au la

Vyama vya upinzani vinasema tatizo kubwa zaidi katika sheria hiyo mpya ni ile hali kwamba inakiuka katiba kwa kutowapatia hifadhi waislam. Vyama vya upinzani vimeshatuma malalamiko yao mbele ya mahakama kuu kudai sheria hiyo ibatilishwe.

Naibu waziri wa mambo ya ndani G.Kishan Reddy anavituhumu vyama vya upinzani kuchochea machafuko na kuongeza kusema kwamba serikali inafanya juhudi za kurejesha nidhamu na sheria.

Waziri mkuu Narendra Modi amevitaja visa vya matumizi ya nguvu kuwa ni vya kuhuzunisha na kutoa wito wa kurejea amani."Matumizi ya nguvu katika maandamano dhidi ya sheria mpya ya uraia yanahuzunisha. Mijadala, mahojiano na maoni tofauti ni sehemu ya demokrasia lakini bila ya kuharibu mali ya umma na kuvuruga hali ya kawaida ya maisha-"amesema waziri mkuu Modi kupitia mtandao wa twitter.

Maafisa wa serikali wamejaribu kuyavunja nguvu maandamano kwa kufunga mawasiliano mtandaoni.

Wito wa kusitishwa machafuko na kurejea kwa amani umetolewa pia na korti kuu inayotarajiwa kuamua kuhusu sheria hiyo mpya ya uraia jumanne.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW