1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano Kenya yatatiza shughuli katika uwanja wa ndege

23 Julai 2024

Maandamano ya Kenya yanayoendelea kwa ajili ya kuishinikiza serikali, yameingia wiki yake ya sita. Kilicho tofauti, ni waandamanaji wanaoiunga mkono serikali kujitokeza katikati ya jiji.

Maandamano Kenya
Maandamano ya kuipinga serikali yaendelea nchini Kenya Picha: Daniel Irungu/EPA

Kwenye kikao cha kwanza cha bunge lililorejea kazini tangu kuanza maandamano ya kudai utawala bora,viongozi walitofautiana juu ya uteuzi wa baraza jipya la mawaziri uliofanyika Ijumaa iliyopita. Junet Mohamed ni kiranja wa upinzani na mbunge wa Suna Mashariki amesisitiza kuwa watakuwa makini sana wakati wa kuwapiga msasa mawaziri wapya.

Rais William Ruto amefanya mabadiliko katika baraza hilo huku Aden Duale na Soipan Tuya wakibadilishana wizara za Ulinzi na Mazingira. Majina 11 ya baraza hilo jipya tayari yamewasilishwa kwa kamati ya uteuzi ya bunge inayotazamiwa kuwakagua na kuandaa ripoti katika muda wa siku 28.
Waandamanaji wanaoiunga na kuipinga serikali wapambana nchini Kenya

Polisi walipambana na waandamanaji kwenye barabara kuu ya kuelekea Mombasa waliokuwa wanajaribu kufika kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA.Maafisa wa kikosi cha wanahewa wanapiga doria kwenye maeneo yanayouzunguka uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA.

Kabla ya hapo, kundi hilo lilikusanyika katikati ya jiji kabla ya kuianza safari yao.Kwenye uwanja wa JKIA kwenyewe, ulinzi ulikuwa mkali kwenye barabara zinazoelekea huko. Kaimu inspekta mkuu wa polisi Douglas Kanja alitahadharisha kuwa uwanja wa kimataifa wa JKIA ni sehemu muhimu inayolindwa na uvamiaji unakiuka sheria.

Maafisa kadhaa walipiga doria kwenye barabara ya Outer Ring ili kuwazuwia waandamanaji kuelekea kwenye uwanja wa kimataifa wa JKIA. Vizuizi vilionekana kwenye sehemu za barabara ya Outer ring na kukagua magari yaliyojaribu kuitumia njia hiyo. Mchana katikati ya jiji la Nairobi, waandamanaji waliobeba mabango walikusanyika wakisisitiza kuwa wao ni wapenda amani.
 

Waandamanaji bado wameapa kujitokeza barabarani licha ya kuzuiwa na Polisi

Waandamanaji bado wameapa kujitokeza barabarani licha ya kuzuiwa na PolisiPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Kundi jengine lilikuwa linaiunga mkono serikali ya rais William Ruto.Baadhi ya mabango yalikuwa na ujumbe unaowataka vijana kukaa pembeni na kumpa Rais Ruto nafasi afanye kazi. Barabara ya kuelekea ikulu ya Nairobi ilikuwa na ulinzi mkali na vizuizi vilidhuhudiwa kwenye sehemu kadhaa. Mjini Mombasa,polisi walilazimika kurusha makopo ya gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwa eneo la Mapembeni kwenye barabara ya Moi.

Ruto asema maandamano Kenya lazima yakomeshwe, upinzani wahimiza 'haki'

Wawili walijeruhiwa kwenye purukushani na kupata huduma ya kwanza hapo kwa papo.Polisi waliendelea kupiga doria mjini na maduka yalifungwa kwa kuhofia usalama wao. Ali Hassan Joho ni gavana wa Mombasa wa zamani na anausisitizia umuhimu wa kusikiliza kilio cha mwenye nchi.

Yote hayo yakiendelea, waandishi wa habari wametangaza kuandamana hapo kesho ili kupinga ukatili wa polisi wanaowatuhumu kwa kuwavamia wakiwa kazini wakati wa maandamano.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW