1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano duniani ukatili wa polisi; kifo cha Floyd

Sekione Kitojo
3 Juni 2020

Jimbo la Minnesota limeanzisha Jumanne uchunguzi wa haki  za  raia  katika  idara  ya  polisi  mjini  Minneapolis kwa  matumaini ya  kulazimisha  mageuzi  kadhaa  kufuatia kifo  cha  George Floyd.

Frankreich Demonstration in Paris in Erinnerung an Adama Traore
Picha: Getty Images/AFP/L. Venance

George Floyd mtu mweusi alifariki  baada  ya afisa wa  kizungu kuibana shingo yake  kwa  goti kwa dakika  kadhaa, hata baada ya  kushindwa kupumua. Wakati  huo  huo  maandamano  kadhaa  yamefanyika katika  miji  mbali  mbali  duniani , ikiwa  ni  pamoja  na  miji ya Ufaransa , Uholanzi, na  Angentina  kupinga  ukatili  wa polisi. 

Gavana wa Minnesota  Tim Walz  na  idara  ya  haki  za binadamu  ya  Minnesota  wametangaza  kufungua malalamiko  rasmi  katika  mkutano  na  waandishi  habari jana  jioni. Gavana  na  kamishna wa  haki  za  binadamu Rebecca Lucero  wamesema  wana  matumaini  kufikia makubaliano  na  mji  huo  kubaini  njia  za  muda  mfupi kuangalia  historia  ya  idara  ya  polisi  ya  ubaguzi wa rangi, na  kutumia  uchunguzi  huo  kupata  suluhisho  la muda  mrefu  kwa  ajili  ya  mabadiliko  ya  mfumo.

Waandamanaji wakiandamna karibu na jengo la mahakama mjini ParisPicha: Getty Images/AFP/M. Rubinel

wakati  huo  huo  mamia  kwa  maelfu  ya  waandamanaji wanaopinga  kifo  cha  George Floyd waliendelea  kubaki katika  mitaa  ya  mjini  New York  jana baada  ya  muda wa   kuanza  kwa  amri  ya  kutotembea  usiku  kuanzia saa  mbili  usiku  saa  za  Marekani, amri  iliyowekwa  na maafisa  ambao  wanahangaika  kuzuwia  uharibifu  pamoja na  malalamiko  yanayoongezeka  kuwa  mji  huo mkubwa nchini  humo  unaingia  katika  hatua  ambayo  hakuna udhibiti  unapoingia usiku.

Meya  Bill de Blasio ameongeza  muda  wa  amri  ya kutotembea  usiku mjini  humo, akiisogeza  kutoka  saa 5 usiku siku  moja  kabla , lakini  alikataa miito ya  rais Donald Trump  na  gavana  Andrew Cuomo  kuleta  kikosi  cha walinzi  wa  taifa.

Maandamano yaendelea

Watu  waliandamana  katika  makundi  ya  maelfu  ya  watu katika  maeneo  ya  Manhatan  na  Brooklyn, wakati  wenye maduka  wakifunga  maduka  yao. Wakati  muda  wa  amri ya  kutotembea  usiku  ulipofika , wengi  walikuwa  bado mitaani  na  waliendelea  kuandamana,  huku  polisi ambao kwanza  walisimama  tu  wakiwaangalia na  kuwaruhusu .

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko MaasPicha: picture-alliance/dpa/J. Schmitz

Mjini  Paris polisi  wa  kutuliza  ghasia  walifyatua  mabomu ya  kutoa  machozi  wakati  waandamanaji  waliokuwa wakitawanyika  wakirusha  vitu  mbali  mbali  na  kuwasha moto wakati  wa  maandamano  ambayo  hayakuidhinishwa dhidi  ya  matumizi  ya  nguvu  ya  polisi pamoja  na ubaguzi wa  rangi. Maelfu  kadhaa  ya  watu  hapo  kabla waliandamana kwa  amani  kwa  muda  wa  masaa  mawili jana  karibu  na  jengo  la  mahakama  mjini  Paris kumuenzi George Floyd  na  Adama traore , Mfaransa mweusi mwenye  asili  ya  Mali  aliyefariki akiwa amekamatwa  na  polisi.

Waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Ujerumani Heiko Maas nae  amesema  maandamano  ya  kupinga  ukatili  wa polisi nchini  Marekani ni  zaidi  ya  kuwa  halali, na kwamba  ana  matumaini  yataleta mabadiliko. Maas ametoa  wito  wa  kuwapo  uhuru  wa  vyombo  vya  habari na  kuwaruhusu waandishi  kufanya kazi  zao  akisema serikali  ya  Ujerumani  itawasiliana  na  Marekani kumuunga  mkono  mwandishi  wa  DW  Stefan Simons ambaye  alishambuliwa  kwa  risasi na  polisi wakati akifanyakazi  yake  ya  kutoa  habari  juu  ya  maandamano mjini  Minneapolis.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW