1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano makubwa tena Hong Kong

Sekione Kitojo
16 Juni 2019

Mamia kwa maelfu ya wakaazi wa Hong Kong, wengi wakivalia nguo nyeusi licha ya hali ya hewa ya joto,waliingia mitaani Jumapili (16.06.2019)katika kuonyesha upinzani wao wa dhati wa sheria kuwapeleka wahalifu China.

Hongkong Massenproteste gegen Regierung
Picha: picture-alliance/dpa/Kyodo

Sheria  hiyo inayopendekezwa  imezusha  hofu  ya  kupanuliwa  udhibiti wa serikali  ya  mjini  Beijing katika  koloni  hilo  la  zamani  la  Uingereza.

Wanaharakati wakishiriki maandamano mjini Hong KongPicha: picture-alliance/epa/A. Hofford

Waandamanaji  wanadai  kwamba  kiongozi  wa  Hong Kong  aufute kabisa mswada wa  kusafirishwa  kwenda  China  bara   ambao utaruhusu  baadhi  ya  watuhumiwa  kupelekwa  kwa  ajili  ya kushitakiwa  katika  China  bara na  kisha  ajiuzulu. Mzozo  huo , ambao  ulitumbukia  katika  ghasia  kubwa  na polisi  wiki  iliyopita, ni moja  kati  ya mtihani mkubwa  wa  hadhi  maalum  ya  eneo  hilo tangu China  kuchukua  udhibiti   baada  ya  kukabidhiwa  mwaka 1997.

Waandamanaji  walibeba   mabango  yanayodai  kuwa  mtendaji mkuu  Carrie Lam ajiuzulu na  hilo likawa kauli  mbiu  iliyokuwa ikiimbwa  mara  kwa  mara  na  waandamanji. Wakitembea  taratibu na  kuimba "ondoa"  na  jiuzulu," kundi  hilo  la  watu  waliijaza  bara bara  kuu  pamoja  na  eneo  la  pembeni  yake  mkabala  na  eneo la  maji  la  bandari  ya  Victoria wakati  watalii  na  wanunuzi  ambao hutembelea  sehemu  hiyo  ya  kitovu cha  biashara  na  fedha katika  eneo  la  asia  wakiangalia.

Waandamanaji wakiweka maua katika eneo alipofariki muandamanaji mmoja aliyekuwa akiweka bangoPicha: AFP/D. De La Rey

Tangazo  la  Lam  siku  ya  Jumamosi  kuwa  anasitisha  sheria  hiyo limeshindwa  kuwatuliza  wakosoaji  wa  hatua  hiyo  ambao wanaiona  kuwa  moja  katika  hatua  ambacho  zinakula uhuru  wa Hong Kong  pamoja  na  sheria  ya mamlaka  yake  ya  ndani.

Hofu ya wapinzani

Wapinzani  wanahofu  kwamba  sheria  hiyo  inaweza  kutumika kuwapeleka  watuhumiwa  wahalifu  nchini  China  na  kuwa  na uwezekano  wa  kukabiliwa  na  mashitaka  yasiyoeleweka  ya kisiasa, uwezekano  wa   kufanyiwa  mateso na  hukumu kinyume  na haki.

"Madai  yetu ni rahisi. Carrie Lam lazima  aondoke  madarakani, sheria  ya  kupelekwa  China  bara  ni  lazima  iondolewe  na  polisi wanapaswa  kuomba  radhi kwa  kutumia  nguvu kubwa  dhidi  ya watu  wake," mfanyakazi  wa  benki John Chow  amesema  wakati akiandamana  pamoja  na  kundi  la  marafiki  zake. "Na tutaendelea."

Moja kati ya mabango yanayoshutumu unyama wa watawala Hong KongPicha: picture-alliance/AP/Kin Cheung

Maandamano  hayo  ya  Jumapili (16.06.2019)  yanaonekana  kuwa katika  kiwango  sawa  na  wiki  moja  iliyopita ambayo  yaliwaleta pamoja  kiasi  ya  watu milioni moja wakielezea  wasi  wasi  wao kuhusiana  na  uhusiano  wa  Hong Kong  na  China  bara. Waandamanaji  walilenga  hasira  zao  kwa  Lam, licha  ya  kukiri kwamba  hana uchaguzi lakini  kuendelea  kupokea  maelekezo yanayotolewa  na  Beijing, ambako  rais Xi Jinping  ameimarisha utawala  wa  mkono  wa  chuma.

Wengi  hapa  wanaamini   haki  ya  mamlaka  ya  Hong Kong imepunguzwa  kwa  kiasi  kikubwa  licha  ya  msisitizo kutoka  Beijing kwamba  bado  inatimiza  ahadi  yake, inayofahamika  kama "nchi moja , mifumo miwili," kwamba  eneo  hilo  linaweza  kuendelea  na mfumo  wake wa  kijamii, kisheria na  kisiasa kwa  miaka  50  baada ya  kukabidhiwa  China  kutoka  Uingereza.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW