1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano makubwa yaitishwa Venezuela

Oumilkheir Hamidou
23 Januari 2019

Wafuasi wa upande wa upinzani na wale wanaoiunga mkono serikali wamepanga kuandamana majiani hii leo nchini Venezuela, siku mbili baada ya kushindwa njama ya wanajeshi ya kutaka kuipundua serikali ya rais Nicolas Maduro.

Venezuela Proteste in Caracas
Picha: Getty Images/AFP/Y. Cortez

 

Wapinzani wa rais wa kijamaa Nicolas Maduro wametolewa wito wa kukusanyika ili kudai "serikali ya mpito" kabla ya uchaguzi mpya kuitishwa."Tuna miadi ya kihistoria na nchi yetu, na maisha ya siku za mbele ya watoto wetu" amesema spika wa bunge Juan Guaido katika kikako cha hadhara cha bunge-taasisi pekee ya nchi hiyo inayodhibitiwa na upande wa upinzani.

Mnamo siku ya pili ya kuapishwa Nicolas Maduro kuendelea na mhula wa pili unaobishwa madarakani, January 11 iliyopita, Juan Guaido alitoa wito wa "kuitishwa maandamano makubwa katika kila pembe ya Venezuela."

Makamo wa rais wa Marekani MIke PencePicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schiefelbein

Marekani inawahimiza wavenezuela wazidi kupaza sauti

 Wito wa spika wa bunge la Venezuela unaungwa mkono pia na makamo wa rais wa Marekani Mike Pence ambaye nchi yake imetangaza vikwazo dhidi ya viongozi wa Venezuela. Katika risala yake kupitia mtandao wa twitter Pence amewataka wananchi wa Venezuela "wahakikishe sauti yao inasikika na kwamba Wamarekani wako pamoja nao."

Rais Nicolas Maduro amejibu kwa kuituhumu Marekani kutaka kuandaa mapinduzi dhidi ya nchi yake. Amemtaka waziri wake wa mambo ya nchi za nje Jorge Arreaza aanzishe utaratibu wa kudurusiwa moja kwa moja uhusiano wa kidiplomasia pamoja na Marekani."

Makamo wa rais Delcy Rodriguez ameituhumu Marekani kuhimiza mapinduzi yafanyike nchini Venezuela.

Spika wa bunge kla Venezuela Juan GuaidoPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Llano

Upande wa upinzani hauna umoja

Ingawa spika wa bunge Guaido anasisitiza katiba inamuunga mkono katika juhudi zake za kumng'owa madarakani Maduro, hata hivyo bunge la Venezuela limepwaya tangu mwaka 2017 pale korti kuu inayodhibitiwa na wafuasi wa Maduro ilipotwikwa madaraka yote ya bunge. Guaido anatambua yote hayo na ndio maana anashadidia anahitaji msaada wa wananchi na jeshi kulifikia lengo hilo.

Wadadisi wanasema upande wa upinzani hauna umoja na changamoto zilizoko ni kubwa. Kipeo cha umashuhuri wake kitabainika leo jumatano, january 23 siku inayoandhimishwa miaka 61 tangu alipotumuliwa madarakani mtawala wa kiimla wa kijeshi Marcos Perez Jimenez.

Wafuasi wa Maduro pia wametakiwa wateremke majiani kubainisha"kipindi cha mpito kinapitia ujamaa" kama anavyosema Diosdado Cabello, mshirika mkakamavu wa Nicolas Maduro.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW