Maandamano mapya Msumbiji yasababisha vifo vya watu saba
16 Januari 2025Rais mpya wa Msumbiji ameahidi kuiunganisha nchi yake iliyogawika vibaya kufuatia uchaguzi uliomuweka madarakani.
Watu saba waliripotiwa kuuawa kufuatia maandamano ya kumpinga kwenye siku ya kuapishwa rais huyo siku ya Jumatano.
Watu hao saba waliouwawa katika mji mkuu Maputo na Nampula, wameifanya idadi ya waliouwawa nchini humo tangu uchaguzi wa Oktoba 9, kufikia watu 307, kwa mujibu wa shirika la Plataforma Decide.
Upinzani bado unashikilia kwamba chama tawala cha Frelimo ambacho kimekuwapo madarakani tangu kumalizika kwa ukoloni wa Kireno mwaka 1975, kiliiba uchaguzi huo uliompa ushindi wa asilimia 65 Chapo.
Uchaguzi huo umetajwa na waangalizi wa Kimagharibi kutokuwa huru wala wa haki, madai yanayokanushwa na Frelimo.
Kiongozi wa upinzani, Venancio Mondlane, ambaye alitangazwa kupata asilimia 24 na Tume ya Uchaguzi, na kurejea nchini Msumbiji wiki iliyopita baada ya miezi kadhaa ya kujificha nje ya nchi, alisema yuko tayari kwa mazungumzo na Chapo.