Maandamano na migomo yaitishia Brazil
3 Juni 2014Makundi ya wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi yamekuwa katika mgomo kwa siku kadhaa, na kutilia mashaka ufanisi wa mashindano hayo ya dunia yanayoanza Juni 12 hadi Julai 13.
Katika mji wa kusini wa Sao Paulo, mgomo wa madereva wa mabasi ulisababisha misongamano mibaya zaidi ya magari kuwahi kushudiwa katika historia ya jiji hilo. Na tarehe 21 Mei karibu askari polisi 8,000 waliandamana mbele ya wizara mbalimbali katika mji mkuu Brasilia, maandamano yaliyoungwa mkono na vikosi shirikisho na polisi jeshi.
Katika miji 12 itakayokuwa wenyeji wa mechi za kombe la dunia, angalau maandamano 15 yamepangwa kufanyika wakati wa ufungunzi wa michuano hiyo. Vyama vya wafanyakazi vinatumia fursa hii ambapo dunia nzima imeelekeza macho nchini Brazil, kuishinikiza serikali ya mrengo wa kati-kushoto ya rais Dilma Rousseff kutekeleza matakwa yao.
Hata wafanyakazi katika balozi za Brazil nchini Marekani na Ulaya waoawajibika kutoa viza kwa wale wanaosafiri kwenda Brazil kwa ajili ya michuano hiyo waligoma wiki iliyopita. Na wafanyakazi wa shirika la ndege la LATAM, ambalo ndiyo kubwa zaidi katika kanda ya Amerika Kusini, lililoundwa kwa kuyaunganisha makampuni ya Tam ya Brazil na Lana la China, walitishia kugoma au kupunguza kasi ya ufanyaji kazi, jambo ambalo linaweza kuathiri shughuli katika viwanja vya ndege na kuvuruga mamia ya safari za kimataifa wakati wa michauano ya kombe la dunia.
Maprofesa katika asilimia 90 ya vyuo vikuu vya taifa na walimu wa shule za msingi za ngazi ya taifa na majimbo wamegoma pia, wakati vituo vingi vya utamaduni na makumbusho vimefunga milango. Katibu mkuu wa chama kikuu cha wafanyakazi nchini Brazil CONDSEF, Sergio Ronaldo da Silva, aliliambia shirika la habari la IPS kuwa hawaondowi uwezekano wa mgomo wa kitaifa.
Ikiwa hali hataibadilika, shughuli katika taifa hilo lenye wakaazi milioni 200 zinaweza kukwama kabisaa wakati wa kombe la dunia, anakiri Ronaldo da Silva baada ya kubainisha kuwa serikali haijapanga tarehe ya kufanya mazungumzo. Aliongeza kuwa wakati mechi za ufunguzi zikikaribia, uhusiano unaweza kushupa zaidi.
Kiongozi huyo wa wafanyakazi anasema serikali ilipaswa kuliona hilo mapema, na kuongeza kuwa inajaribu kuonyesha taswira ya Brazil kama taifa la ulimwengu wa kwanza, wakati mifumo sekta za kijamii kama vile afya, elimu na usafiri ikiwa karibu haifanyi kazi tena. CONDESF inawakilisha karibu asilimia 80 ya wafanyakazi wa umma milioni 1.3. Ronaldo da Silva alisema tarehe 30 Mei watajadili uwezekano wa mgomo wa kitaifa katika shirikisho lao.
Mwishoni mwa mwaka wa 2013 serikali ilisaini zaidi ya mikataba 140 ya kazi na vyama mbalimbali vinavyowawakilisha wafanyakazi, ikiahidi miongoni mwa mambo mengine nyongeza ya asilimia 15.8 itakayolipwa katika robo tatu za kila mwaka. Lakini vyama vinalalamika kwamba wakati huo, kiwango cha mfumuko wa bei kilikuwa kidogo kuliko cha sasa cha asilimia 26, na Ronaldo da Silva anasema kati ya mikataba iliyosainiwa, asilimia 70 bado haijatimizwa.
Tangu Februari 2012 bunge limekuwa likijadili mapendekezo ya kuzuwia migomo wakati wa kombe la dunia. Mswada wa sheria uliyopo mbele ya bunge la seneti, utadhidbiti maandamano kabla na wakati wa michuano hiyo. Chini ya sheria hiyo, vyama vitapaswa kutangaza mgomo siku 15 kabla, na kwamba asilimia 70 ya wafanyakazi laazima wabaki kazini.
Wakati Brazil ilipoteuliwa kuwa mwenyeji wa kombe la dunia la mwaka huu, hakuna aliefikiria kuhusu maandamano, kwa sababu asilimia 80 ya raia walikuwa wanaunga mkono juhudi za nchi hiyo kuandaa mashindano hayo. Lakini hivi sasa asilimia 55 ya waliohojiwa wanasema kombe la dunia litailetea Brazil matatizo zaidi kuliko manufaa.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ips
Mhariri: Josephat Charo