Maandamano ya Cologne na uchaguzi wa Ukraine magazetini
27 Oktoba 2014Tuanze lakini na mandamano ya makundi ya wahuni wafanya fujo walioshirikiana na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia katika eneo la kati la jiji la Cologne.Gazeti la "Westfälische Nachrichten" linaandika:"Ni mchangayiko hatari kabisa!Wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na makundi ya wafanyafujo wasiohofia kutumia nguvu wameunda ushirika wa vitisho.Jamii itarajie kitu gani?Kwa upande mmoja visa vinavyozidi vya makundi ya itikadi kali ambayo wafuasi wake hawafikirii chengine isipokuwa kuteremka vitani.Na kwa upande wa pili makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia na mashabiki wa dimba wasiohofia kutumia nguvu,walioamua kuungana ili kuendeleza mapambano dhidi ya itikadi kali ya dini ya kiislam.Serikali inabidi iwe macho,isije ikashindwa kuidhibiti hali ya mambo.
Maoni sawa na hayo yameandikwa pia na gazeti la "Hannoversche Allgemeine "linalohisi mashabiki wanaofanya fujo wa dimba,azma yao si kuiokoa dunia toka kitisho cha wafuasi wa itikadi kali-wao wenyewe ni kitisho.Gazeti linaandika:"Si bahati nasibu kwamba hivi sasa mahasimu hao wa jadi,yaani wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na mashabiki wa dimba wafanyafujo,wameungana.Sehemu kubwa ya mashabiki hao wa dimba wasiohofia kutumia nguvu wanashirikiana na wanazi mambo leo na wafuasi wengine wa siasa kali za mrengo wa kulia wanaotumia kitisho kinachosababishwa na wanamgambo wa dola la kiislam IS ili kuchochea hisia za kale.Ushirika dhidi ya itikadi kali ya dini ya kiislam unakwenda mbali zaidi.Hata makundi ya muziki wa Rock &Roll wameunga mkono maandmano ya Cologne.Kilichosalia ni kutaraji tu kwamba vuguvugu hilo halitazaa ushirika wa matumizi ya nguvu dhidi ya kila anaefuata imani ya kiislam.Kwasababu watakaotishwa na vuguvugu kama hilo si wanamgmbo wa IS bali wajerumani wa kawaida.
Masikilizano pamoja na Urusi ni muhimu
Mada yetu ya mwisho inahusu uchaguzi wa bunge nchini Ukraine.Vyama vinavyoelemea upande wa magharibi vimeshinda.Matokeo hayo hayaibadilishi hali tete iliyoko nchini humo,linaandika gazeti la "Nordbayerische Kurier":Wakaidi nchini Ukraine bado wanatafuta malumbano pamoja na Moscow."Tunaelekea Brussels"-ndio kauli mbiu yao.Lakini mama ambao watoto waao wamefariki katika uwanja wa vita mashariki ya nchi hiyo wanapendelea masikilizano pamoja na Urusi ili kusitisha umwagaji damu.Ushupavu utakapokoma ndipo busara itakapotawala.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Saumu Mwasimba