Maandamano ya kumbukumbu katika kambi ya mateso ya Auschwitz,Poland.
5 Mei 2005Treni sita maalum zilizokodiwa na mabasi kadhaa yalianza kuwasili mapema leo huko Oswiecim.Umati huo wa watu uliweza kuingia katika kambi hiyo iliyokuwa ya mateso huku wakisubiri kuanza kwa maandamano yao.Kiasi cha watu 18,000 hadi 20,000 wanakadiriwa kuhudhuria maandamano hayo wakitokea nchi 50.
Miongoni mwao akiwemo Parisian Jonathan Gottlieb mwenye umri wa miaka 21,ambaye ana asili ya Poland na Kiyahudi,huyo alimpoteza babu yake aliyeitwa Haim katika mauaji ya Holocaust na amebeba picha ya babu yake huyo.
Kijana huyo amesema kuwa alipokuwa ndani ya treni alikuwa anajiuliza ilikuwaje wafungwa waliopelekwa katika kambi ya mateso ya Auswitz walivyomudu kuishi katika kambi hiyo.
Waandamanaji hao wametoka Australia,Canada,Ugiriki,Mexico,Marekani,Poland,Afrika Kusini na kwengineko.Kundi hilo la waandamanaji linajumuisha vijana na wazee,Wayahudi na wasio Wayahudi,wote wakiwa wamejiandaa kuelekea Birkenau,sehemu ya kambi hiyo kwa ajili ya kuwakumbuka waliopata madhila makubwa katika mauaji ya Holocaust.
Jurek Sternfeld mwenye umri wa miaka 66 sasa,alizaliwa Warsaw Poland miezi sita kabla ya majeshi ya manazi wa Ujerumani hawajaivamia Poland,kuanza vita vikuu vya pili vya dunia,ambavyo ni njanga lisilosemekana kuwahi kutokea katika historia ya dunia hii.Familia yake ilinusurika katika vita hivyo baada ya kutorokea Urusi mwezi wa Septemba mwaka 1939.Kwa sasa anaishi Australia.
Anaeleza kuwa hili ni jambo muhimu hasa ikizingatiwa mustakabali wa baadae wa dunia hii unavyotazamwa,kuweza kukumbuka kile kilichotokea.Sternfeld anaendelea kueleza kuwa ni jambo baya sana lililowahi kutokea katika historia ya binadamu.Akifikiria jinsi kundi kubwa la watu lilivyoweza kuangamizwa lote.
Anaeleza kuwa jambo kama hilo lisiruhusiwe kutokea tena duniani na ndio sababu iliyomfanya kufika katika maandamano hayo.
Katika kumbukumbu hizo waandamanaji hao wanatazamiwa kusikiliza hutuba kutoka kwa Waziri Mkuu wa Israel,Ariel Sharon,Waziri Mkuu wa Poland Marek Belka na mfungwa wa zamani katika kambi ya Auschwitz,msomi wa Kiyahudi na mwandishi wa vitabu Elie Wiesel,wote hao wakiwa wanatazamiwa kutoa ujumbe wa wajibu wa dunia kukumbuka mauaji ya Holocaust na kuweka mkazo yasipewe nafasi kutokea tena.
Inakadiriwa kiasi cha watu milioni 1 na laki moja,wanaume,wanawake na watoto wengi wakiwa Wayahudi walikufa katika kambi ya mateso ya Auschwitz-Birkenau,eneo ambalo lilihesabika kuwa kituo cha mwisho cha ukatili wa Manazi wa Kijerumani,ambao walikuwa na nia ya kuwafuta katika ramani ya dunia Wayahudi wa Ulaya milioni 11.
Kikundi cha waalimu wa kanisa Katoliki kutoka Marekani wameonekana wamejipanga nje ya lango la kuingilia katika kambi hiyo,wakisubiri ukaguzi wa walinda usalama.
Waalimu hao wamesema hii ni nafasi yao nao kushiriki maandamano hayo,ili kuonesha wanakumbuka miaka 60 ya kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia.
Majeshi ya Manazi yaliwauwa Wayahudi wa Ulaya milioni sita,nusu yao wakitoka madhehebu ya Wakatoliki wa Poland,mahali ambapo Jumuia ya Wayahudi wengi wa Ulaya walikuwa wakiishi kabla ya kuanza vita vikuu vya pili vya dunia. Maandamano kama hayo yakuigutusha dunia juu ya madhila kama hayo yasitokee tena,yalianza tangu mwaka 1988 kwa kuwashirikisha vijana wa Kiyahudi pekee,lakini kadri siku zilivyokuwa zinakwenda,yameweza kuwa kivutio pia kwa watu wazima,walionusurika mauaji hayo,wanafunzi na katika miaka michache iliyopita yameweza kuwavuta hata watu wasiokuwa Wayahudi.