1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya kupinga uchaguzi Msumbuji yageuka vurugu

Angela Mdungu
25 Oktoba 2024

Mji mkuu wa Msumbiji wa Maputo umekumbwa na vurugu siku ya Ijumaa, wakati maandamano ya usiku kucha yakigeuka kuwa ya ghasia kufuatia chama tawala cha Frelimo kuchaguliwa tena baada ya miaka 49 madarakani.

Msumbiji I Waandamana kupinga matokeo ya uchaguzi katika wilaya ya Maxaquene
Waandamanaji kutoka kitongoji cha Maxaquene wakikabiliana na vikosi vya usalama vya Msumbiji walipokuwa wakiandamana mjini Maputo Oktoba 24, 2024.Picha: Alfredo Zuniga/AFP

Mamia ya wafuasi wa upinzani waliandamana, wakikataa kile walichokitaja kuwa kura iliyoporwa na tume ya uchaguzi "fisadi". Tume hiyo ilimtangaza mgombea wa Frelimo Daniel Chapo kushinda uchaguzi wa Oktoba 9 kwa asilimia 71 ya kura. Waandamanaji wamechoma moto matairi ya magari, kuziba njia mjini Maputo na kuharibu mabango ya uchaguzi ya Frelimo. Baadhi yao waliwarushia mawe polisi, ambao walirusha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya, kwa mujibu wa ripota wa AFP. Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane aliyejitangaza kuwa mshindi amedai uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu na kuitisha maandamano.