Maandamano ya kupinga safari ya mwenge wa Olimpiki
8 Aprili 2008Katika maoni yao hii leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia safari ya mwenge wa michezo ya Olimpiki na mzozo unaoikbali benki ya mikopo ya Ujerumani.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linasema machafuko yaliyotokea dhidi ya mwenge wa Olimpiki mjini London Uingereza na Paris nchini Ufaransa ni taswira ya tatizo zima linalokabili moyo wa kuipenda michezo ya Olimpiki. Hata rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki, Jacques Rogge, kufikia hivi sasa hakuwa na uhakika kuhusiana na swala hilo.
Iwe ni kejeli kwa Tibet au hila dhidi ya michezo ya Olimpiki, ni jambo ambalo haliwezi kukanushwa kwamba siasa na michezo viko katika kapu moja ikiwa mataifa yanataka kupitia msaada wa mwenge wa Olimpiki kudhihirisha na kudumisha amani.
Wapinzani wa michezo ya Olimpiki wamekufanya kuuzima mwenge wa Olimpiki kuwa aina fulani ya mchezo. Mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung anasema hii ni aina ya kipekee ya mchezo ambapo kuna wachezaji wa kutumia midomo.
Hisia za China
Gazeti la Tageszeitung linatupia jicho hisia za China. Serikali ya China mjini Beijing inazungumzia kuwepo na njama ya kuihujumu.
China ilitaka kuitumia michezo ya Olimpiki kujitangaza kwa ulimwengu kwa hali nzuri kabisa kadri ya uwezo wake. Sasa ikiwa haiwezi kusema lolote, inalazimika kutazama pia jinsi sheria zinavyokiukwa nje ya mipaka yake.
Wakiwa hawana la kufanya maafisa wa serikali ya China wanatazama maandamano dhidi ya mwenge wa Olimpiki mjini London na Paris ambayo yanatarajiwa kuonekana pia huko San Franscisco Marekani na New Delhi nchini India.
Mhariri wa gazeti la Tageszeitung anamalizia kwa kusema safari ya mwenge wa Olimpiki itageuzwa kuwa chombo cha kisiasa, hatua ambayo itaharibu taswira ya mwenge huo katika kila kilomita itakayosafiri.
Gazeti la Thüringische Landeszeitung la mjini Weimar linasema maafisa wa michezo nao pia wamelazimika kutazama machafuko yanayoendelea dhidi ya mwenge wa Olimpiki wakiwa hawana la kufanya.
Waandamanaji wa London na Paris walitaka tu kutoa funzo kuhusu ukiukaji wa haki za biandamu unaofanywa na China katika jimbo la Tibet. Kwa mtazamo wake mhariri wa gazeti la Thüringische Landeszeitung anasema waandamanaji hao wanalinda wazo na lengo la michezo ya Olimpiki na wala sio maafisa wa michezo ambao wameifanya michezo ya Olimpiki kuwa maonyesho ya kibiashara.
Mzozo wa benki
Mada ya pili iliyozingatiwa na wahariri hii leo ni mzozo unaoikabili benki ya mikopo ya serikali ya Ujerumani na kujiuzulu kwa mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Matthäus-Maier.
Gazeti la Süddeutsche Zeitung linasema kuondoka kwa Matthäus-Maier kunatoa uhuru mpya wa kufanyika mazungumzo baada ya benki hiyo ya mikopo kupitia mpango wake wa kuiokoa benki ya kutoa mikopo ya muda mrefu kwa kampuni za wizani wa kati ya IKB kushindwa kufaulu.
Matthäus-Maier alitoa mikopo liyopunguzwa kwa kampuni ndogo, wajenzi wa nyumba za kibinafsi au hata wanafunzi. Hilo aliweza kulifanya kwa sababu alipata fedha kiurahisi katika soko, lakini benki ya mikopo ya serikali ya Ujerumani haipaswi kulipa gharama za makosa yake.
Kuondoka kwa Matthäus-Maier, mtaalamu wa zamani wa maswala ya fedha wa chama cha Social Democratic, SPD, hakusaidii sana, linasma gazeti la Märkishce Allgemeine la mjini Potsdam.
Mhariri wa gazeti hilo anasema benki ya serikali ya kutoa mikopo, inakaribia kuishiwa na fedha. Bila kujali nani atakayechukua wadhifa wa Matthäus-Maier, kiongozi mpya atalazimika kutafuta hatua za haraka kuinusuru benki hiyo ya serikali kutokana mzozo mkubwa unaoikabili.