Maandamano ya kupinga ufisadi Serbia yageuka machafuko
14 Agosti 2025
Haya yanafanyika wakati miezi ya maandamano ya kuipinga serikali yamegeuka na kuwa machafuko kwa usiku wa pili mfululizo. Waandamanaji wanaopinga ufisadi walikusanyika katika miji kote nchini Serbia usiku wa Jumatano na ni kutokana na uvamizi uliofanywa na wafuasi wa chama tawala dhidi ya waandamanaji katika mji wa Vrbas, karibu kilomita 160 kaskazini mwa Mji Mkuu Belgrade.
Waandamanaji wanaoiunga mkono serikali wakiwa wamevalia barakoa, walikabiliana na wenzao wanaoipinga serikali na kurushiana chupa, mawe na fataki.
Polisi iliwakamata karibu watu 50 kote nchini humo na takriban polisi 30 walijeruhiwa.
Machafuko mabaya zaidi yameripotiwa katika miji ya Belgrade na Novi Sad ambako vuguvugu la maandamano hayo lilianza.
Mtu mmoja ambaye baadae alitambuliwa kama afisa wa polisi alifyatua bastola hewani wakati waandamanaji walipokuwa wakielekea katika afisi za chama tawala mjini Novi Sad, na kusababisha taharuki.
Kumekuwa na wimbi la maandamano ya kupinga ufisadi nchini serbia tangu mwezi Novemba, wakati kuporomoka kwa kituo cha treni cha Novi Sad kuliposababisha vifo vya watu 16, tukio lililohusishwa na ufisadi uliokita mizizi nchini humo.