1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya kudai mageuzi nchini eSwatini yageuka vurugu

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
29 Juni 2021

Waandamanaji katika nchi ndogo ya kusini mwa Afrika ya eSwatini wameingia barabarani kudai mageuzi katika mfumo wa utawala ambao kwa sasa nchi hiyo inatawaliwa na mfalme Mswati wa Tatu.

Swasiland:  König Mswati III bei einer Traditionsveranstaltung
Picha: picture-alliance /dpa/J. Bätz

Watu nchini Eswatini wanaandamana kutaka mageuzi katika mfumo wa utawala wa nchi hiyo ya kifalme ya kusini mwa Afrika. Kwenye nchi hiyo mfalme ndiye mwenye mamlaka takriban yote. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari mfalme Mswati wa Tatu amekimbilia katika nchi jirani ya Afrika kusini. Hata hivyo msemaji wa serikali Sabelo Dlamini amekanusha habari hizo kwamba Mfalme Mswati wa Tatu amekimbia kutoka nchini humo na kwenda nchi jirani ya Afrika Kusini.

Ghadhabu dhidi ya mfalme Mswati imekuwa inatokota kwa muda wa miaka mingi na maandamano yaliyofanyika yaliakisi ghadhabu hiyo. Waandamanaji walifanya ghasia za hapa na pale na polisi walitumia gesi ya kutoa machozi, na risasi za moto pamoja na maji ya kuwasha ili kuwatawanya wananchi waliokuwa wanawatupia mawe.

Wanaharakati wamesema mfalme Mswati wakati wote amejaribu kukwepa miito juu ya kuleta mageuzi ya kuielekeza nchi yake kwenye lengo la demokrasia. Wananchi hao pia wamemlaumu mfalme kwa kula fedha za umma kwa ajili ya kugharamia maisha yake ya anasa bila ya kuzingatia gharama za wananchi wake wapatao milioni 1.5. 

Mfalme Mswati lll wa eSwatini na mmoja kati ya wake zake, Inkhosikati LaMbikizaPicha: Getty Images/AFP/K. Sahib

Hadi kufikia jana jioni, moja wapo ya maduka makubwa nchini Eswatini, duka la "OK Foods", pamoja na maduka mengine, yalichomwa moto wakati wa maandamano hayo ya watu wanaounga mkono demokrasia ambayo yaligeuka na kuwa machafuko. Hili ni tishio la kwanza kwa mfalme Mswati wa Tatu ambaye ametawala nchi hiyo ya kusini mwa Afrika bila kukabiliwa na bughdha za aina yoyote. Lakini katika siku za hivi karibuni nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na maandamano kwa siku kadhaa katika maeneo yasiyopungua 10, hali iliyowalazimisha polisi kuwatawanya waandamanaji.

Mnamo siku ya Ijumaa polisi walipambana na mamia ya waandamanaji vijana walioshiriki kwenye maandamano ya kupinga utawala wa kifalme katika nchi hiyo pekee barani Afrika iliyobaki na utawala wa kifalme katika mji wa Msunduza, ulio karibu na mji mkuu wa Eswatini, Mbabane.

Msemaji wa kundi linalounga mkono demokrasia la Swaziland Solidarity Network, Lucky Lukhele, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanajeshi wamemwagwa barabarani na kwamba usiku wa kuamkia leo kijana mmoja alipigwa risasi na jeshi na wengine wako hospitalini.

Mfalme Mswati lll alipohutubia katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New YorkPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Franklin II

Serikali ya Eswatini wiki iliyopita ilipiga marufuku maandamano, huku Kamishna wa Polisi nchini humo William Dlamini akionya kwamba maafisa wake hawatastahimili kabisa ukiukaji wa marufuku hiyo.

Mfalme, Mswati wa Tatu aliyetawazwa na kuvikwa taji la ufalme mnamo mwapa 1986 alipokuwa na umri wa miaka 18 tu, amekosolewa kwa matumizi yake binafsi yenye gharama kubwa wakati raia wengi nchini mwake wakiwa wanaishi katika hali ya umaskini.

Mfalme Mswati wa Tatu amekanusha madai kuwa yeye ni dikteta na wala hana la kutahayari juu ya wake zake 15 ambao pamoja na yeye mfalme wanamiliki makasri kadhaa yanayolipiwa kwa fedha za umma. Hatua zilizochukuliwa na serikali kuwasaka viongozi wa upinzani pamoja na kuwatia ndani mnamo mwaka 2019  hazikusaidia kuzima hisia za kuuchukia utawala wa mfalme Mswati wa Tatu.

Vyanzo:/RTRE/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW