1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yasimamisha shughuli katika mji mkuu wa Guinea

29 Julai 2022

Maandamano ya kuupinga utawala wa Guinea na jinsi unavyoshughulikia mchakato wa kurejesha demokrasia nchini humo, yamesababisha kusimama kwa shughuli katika mji mkuu wa nchi hiyo, Conakry.

Guinea | FNDC Demonstrationen
Picha: CELLOU BINANI/AFP/Getty Images

Waandalizi wa maandamano hayo wamedai kuwa mtu mmoja ameuawa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mfungamano wa kitaifa wa ulinzi wa katiba, FNDC, mtu huyo aliuliwa kwa kupigwa risasi na watu wengine kadhaa walijeruhiwa. Mfungamano huo wa kisiasa wenye ushawishi mkubwa nchini Guinea uliandaa kampeni hiyo ya upinzani ili kushutumu uamuzi uliofanywa na utawala wa Guinea ya Conakry juu ya kuudhibiti mchakato wa kurejesha utawala wa kiraia, baada ya kutwaa madaraka mwaka uliopita.

Waandamanji mjini Conakry katika maandamnao yaliyoandaliwa na FNDCPicha: CELLOU BINANI/AFP/Getty Images

Mpaka sasa watawala wa nchi hiyo hawajasema chochote juu ya kifo cha mtu huyo aliyepigwa risasi. Mfungamano wa kulinda katiba umewalaumu watawala wa kijeshi wa Guinea kwa kukataa kuanzisha mdahalo wa dhati juu ya kufafanua utaratibu wa kurejesha demokrasia.

Wakati huo huo mwendesha mashtaka wa serikali amewaagiza mawakili wa sehemu kadhaa kuwachukulia hatua za kisheria walioandaa maandamano ya mjini Conakry yaliyokuwa yamepigwa marufuku. Machafuko yalizuka kati ya waandamanaji na polisi kwenye sehemu kadhaa zinazozingatiwa kuwa ngome za wapinzani katika mji mkuu,Conakry. 

Kushoto: Rais wa Guinea Bissau, Umaro Sissoco Embalo. Kulia: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Mwenyekiti wa jumuiya ya uchumi ya Afrika magharibi ECOWAS Umaro Sissoco Embalo ambaye pia ni rais wa Guinea Bissau amewataka watawala wa kijeshi nchini Guinea waharakishe hatua za kurejesha demokrasia. Embalo amesema alikutana na viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo hivi karibuni ili kuwaelewesha juu ya uamuzi wa wakuu wa nchi wa jumuiya ya Ecowas wanaotaka mchakato wa kurudishwa utawala wa kiraia nchini humo usivuke muda wa miaka miwili ingawa kanali Mamady Doumbouya aliyeiangusha serikali ya rais Alpha Conde mwaka uliopita aliahidi kurejesha mamlaka kwa raia katika muda wa miaka mitatu. 

Rais huyo wa Guinea Bissau ambaye pia ni mwenyekiti wa jumuiya ya uchumi ya Afrika magharibi ECOWAS Umaro Sissoco Embalo amesema katika mkutano na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron siku ya Alhamisi kwamba Guinea ya Conakry itakubali kupunguza kipindi cha mpito cha utawala kuelekea utawala wa kiraia kutoka miaka mitatu hadi miwili.

Kanali Mamady Doumbouya aliyeiangusha serikali ya rais Alpha Conde mwaka uliopitaPicha: Xinhua/imago images

Amesema katika siku za hivi karibuni yeye na waziri wake wa mambo ya nje watakwenda nchini Mali kuonana na viongozi wa kijeshi amesema ana imani watafikia muafaka kwa sababu ni muhimu pia kukimaliza kipindi cha mpito nchini Mali.

Chanzo:AFP

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW