1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya mazishi ya Soleimani yafanyika Baghdad

Sylvia Mwehozi
4 Januari 2020

Maelfu ya raia wa Iraq, wakiwemo wanasiasa wamehudhuria maandamano ya mazishi mjini Baghdad siku ya Jumamosi, ya Jenerali wa ngazi ya juu wa Iran na wapiganaji wengine waliouawa katika shambulio la anga la Marekani.

Irak Bagdad Trauermarsch für Kassem Soleimani und Abu Mahdi al-Muhandis
Picha: Reuters/W. al-Okili

Shambulio hilo la Alhamis jioni karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad lilimuua Qassem Soleimani, kamanda wa jeshi la Iran la Quds pamoja na Abu Mahdi al-Mohandes, naibu mkuu wa jeshi la wanamgambo la Iraq la Hashd al-Shaabi sambamba na wapiganaji wengine walio na mafungamano na Iran.

Maandamano ya mazishi

Siku ya Jumamosi, miili ya wale waliouawa kwenye shambulio hilo ilibebwa katika magari ya kijeshi katika maandamano ya mazishi iliyoongozwa na wapiganaji wa Iraq waliokuwa wamebeba bendera za Iraq na mabango ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran. Waziri mkuu wa Iraq Adel Abdel-Mahdi na Hadi al-Amiri ambaye ni kiongozi mwandamizi katika kundi la Hashd al-Shaabi wamehudhuria maandamano hayo.

Waombelezaji walio na hasira walipaza sauti za kuipinga Marekani na kutaka hatua za kulipiza kisasi. "Kifo kwa ajili ya Marekani", baadhi ya waombolezaji walipaza sauti, wakati helkopita za jeshi la Iraq zikipiga doria angani kama sehemu ya kuimarisha usalama.

Wengi wa waombolezaji walivalia nguo nyeusi na kubeba bendera za Iraq pamoja na bendera za wanamgambo wanaoungwa mkono na Iranambao ni watiifu kwa jenerali Soleimani.

Gari iliyoubeba mwili wa Qassem SoleimaniPicha: AFP/S. Arar

Maandamano hayo ya mazishi yalianzia katika kaburi la Imam Kadhim mjini Baghdad, moja ya eneo takatifu kwa Washia wa Kiislamu. Mmoja ya waombelezaji aliyevalia nguo nyeusi, Mohammed Fadl amesema mazishi hayo ni ishara ya utiifu kwa viongozi hao waliouwa. "Ni shambulio la kuumiza, lakini halitotutikisa".

Kulingana na jeshi la wanamapinduzi la Iran, mwili wa kamanda Qasem Soleimani utazikwa siku ya Jumanne katika mji alikozaliwa wa Kerman kama sehemu ya siku tatu za maombelezo ya nchi nzima. Mwili wake ulitarajiwa kuwasili mjini Tehran usiku wa Jumamosi kabla ya kupelekwa katika mji mtakatifu wa Mashhad siku inayofuata kwa ajili ya ibada ya mazishi itakayofanyika katika kaburi la Imam Reza.

Marekani, Uingereza zaamuru raia wake kuondoka

Marekani imewaamuru raia wake kuondoka Iraq na kufunga ubalozi wake mjini Baghdad. Serikali ya uingereza nayo siku ya Jumamosi, ilitoa onyo kwa raia wake kutosafiri kuelekea Iraq au kufanya safari za aina yoyote kuelekea Iran kufuatia kuuwawa kwa Qassem Soleimani, Kamanda wa kijeshi wa ngazi ya juu wa Iran.

Afisi ya Wizara ya mambo ya kigeni imesema kufuatia mvutano wa kikanda unaozidi kupamba moto, hivi sasa imewashauri raia wake kutosafiri kuelekea katika maeneo hayo isipokuwa tu eneo la Kurdistan. Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Dominic Raab amesema ni vizuri raia wa taifa hilo kufikiria kwa makini iwapo ni salama kwao kusafiri kuelekea Iran kwa sasa.

Afghanistan nayo yaelezea wasiwasi

Afghanistan imeelezea wasiwasi wake juu ya uwezekano wa kuongezeka vurugu za kikanda kufuatia shambulio la Marekani lililomuua Generali mkuu wa Iran Qassim Soleiman. Kulingana na taarifa kutoka kwa taifa hilo linalokumbwa na vita, limetoa wito kwa jirani yake Iran na mshirika wake wa kimkakati Marekani kujizuia ili kuepusha mgogoro kupanuka zaidi.

Kamanda Qassem Soleimani alyeuawa na MarekaniPicha: picture-alliance/dpa/AP/E. Noroozi

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani aliandika katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter kwamba amezungumza na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo na kumueleza kuwa Afghanistan haiwezi kutumika dhidi ya taifa lingine au kuanzisha mgogoro wa kikanda. Kwa upande wake kiongozi Mkuu wa Serikali ya Afghanistan Abdulla Abdulla amesema anatumai matukio ya hivi karibuni hayatakuwa na athari mbaya kwa ushirikiano kati ya marafiki na washirika wa Aghanistan.

Soleimani alikuwa akichukuliwa kama moja ya viongozi wa kijeshi walio na nguvu nchini Iran, akiwa na ushawishi katika nchi za Iraq, Syria na baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati ambako Iran imekuwa na shughuli zake za kijeshi.

Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ametishia kulipiza kisasi kwa Marekani kufuatia mauaji ya Soleimani. hata hivyo rais Donald Trump ametetea uamuzi wa kumuua Soleimani akisema amechukua hatua za "kuzuia vita". Utawala wake umesema kamanda huyo alikuwa akipanga mkururo wa mashambulizi ambayo yalihatarisha vikosi vya Marekani na maafisa wake, bila ya kutoa ushahidi wa hilo.